Nchini ya Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, lugha ya
Kiswahili imekuwa nyenzo muhimu katika kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani
ya Umoja wa Mataifa, ikitumiwa na walinda amani wa chombo hicho hususan wale
wanaotoka Tanzania, sambamba na raia.
Mashuhuda wa
Kiswahili na ulinzi wa amani ni walinda amani wa Tanzania wa kikundi cha 7,
TANZBATT 7, cha kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha ujumbe wa Umoja wa
Mataifa nchini DRC, MONUSCO.
Meja Michael
Kibira ni miongoni mwao mjini Beni jimboni la Kivu Kaskazini na anasema kuwa,
"lugha ya kiswahili imekuwa ikiongelewa katika eneo hili la Kivu kaskazini
na raia wengi kuanzia wadogo ni lugha yao ambayo wanakua nayo.
“Na sisi
tunaitumia kama ni faida kwetu kwa sababu unapokuwa unakutana na raia wa DR
Congo unakuwa uko huru kuongea naye, naye anakuamini.
“Unajua
katika maeneo ya vita, yule ambaye ni mwaathirika wa vita anakuwa ni mtu ambaye
anatilia shaka kila mtu ambaye ni mgeni kwake.
“Hapa DR
Congo tumekuwa tukifanya kazi na mataifa mbalimbali kuna Malawi, Afrika Kusini
na Indonesia."
Mlinda amani
huyu kutoka Tanzania anatoa mfano zaidi akisema kuwa, "kwa mfano hapa ninafanya kazi na mtu
kutoka Indonesia,
“kwa hivyo
wakikutana na mtu ambaye ni raia wa Indonesia
ni tofauti kabisa na wanavyokutana na sisi kwasababu wanapokutana na
mimi wanakuta kwamba sihitaji kuwa na yule msaidizi wa lugha.
“Mimi, ana
uwezo wa kunisongelea, akaongea na mimi ni kama ndugu moja na anatambua kabisa
kwamba nyinyi Tanzania ni ndugu zetu tunaongea lugha moja,
“tunafahamiana
hata kama lugha yangu mimi wa DRC haijanyooka kama Kiswahili chenu lakini tunaelewana vizuri.
“Kwa hivyo
mimi hapa Kamango nimeitumia kama silaha ambapo naweza nikaambiwa kitu kama
akiona adui anakwambia kule rafiki usiende kuna hii na hii kwa hivyo mimi
nasema hiyo ni silaha na msaaada mkubwa sana kwetu watanzania kufanya kazi hapa
Congo!"
Kwa upande
wake Kepteni Salum Lihega, lugha ya Kiswahili inafanikisha doria kama akifafanua
kuwa, "lugha ya Kiswahili imetoa msaada mkubwa sana kwetu kwasababu
imeleta urahisi sana katika kuwafikia raia na kufanya nao mazungumzo
mbalimbali.
“Lugha ya
Kiswahili imeenea na hii imepelekea kutuletea urahisi sana sisi katika
kuwafikia raia kuzungumza nao kupata taarifa mbalimbali na pia sisi kujenga nao
mahusiano yaliyo karibu.
“Kuna suala
moja ambalo kwa kweli naomba nilizungumze nitoe pongezi zangu za dhati kwa
wasanii wetu wa Tanzania waimbaji wa nyimbo za injili na vile vile hata
waimbaji wa hizi nyimbo za kizazi kipya nao wamechangia sana katika kueneza hii
lugha ya Kiswahili katika nchi hii.
“Utasikia
nyimbo za injili kama vile za Rose Mhando, na
Christina Shusho na vile vile za kizazi kipya kama vile za Diamond
Platnumz na Ali kiba. Sasa hivi nikipita huko mitaani huona sisi tunapita
kuzungumza nao na hasa hasa wakizisikiliza zile nyimbo na kutuona sisi wanaona
kwamba sisi ndio wale ambao tumekuwa tukiziimba zile nyimbo.
“Kwa kweli
imeleta faraja sana kwa watanzania tujidai kuwa na kiswahili tujivunie,
tukitetee Kiswahili tukilinde na tujitahidi kukikuza ili kiweze kuenea sehemu mbalimbali ukiacha hapa DRC."
Kinasaidia
kupata taarifa kutoka kwa tunaowalinda
Walinda
amani hao kutoka Tanzania wanaendelea kuelezea ni kwa vipi wakiwa wanasaka
taarifa za ulinzi wa amani, lugha ya Kiswahili ni nyenzo muhimu ambapo Luteni
Godfrey Mzungu anasema kuwa,
"Niko
huku katika ulinzi wa amani katika kuongoza doria mbalimbali kwa maeneo ya DRC
na nimekuwa katika hili jukumu kwa maeneo ya Beni, Mavivi lakini pia nimekuwepo
katika majukumu katika sehemu moja inatwa Matombo.
“Mfano
mzuri, mimi katika eneo la Sake katika doria zangu najitahidi kukutana na raia
wengi tunaongea lugha vizuri ni tofauti kati ya majirani wenzetu ambao wapo
katika hili jukumu inaleta shida sana katika kuwasiliana na raia, inafikia
kipindi mpaka wawe na mtu anayetafsiri.
“Lakini sisi
raia wanatueleza shida zao mbalimbali tunakutana na machifu wao wanatufikishia
habari mbalimbali ambazo zinasaidia kabisaa katika utendaji kazi wetu."
Kwa upande
wake Sajini Nassoro Mohammed anasema kuwa , "Kiswahili kimetusaidia sana
kwa ndugu zetu wacongo kuleta umoja katika DR Congo, kwa hiyo tunasaidia sana
na wanapenda sana tuongee Kiswahili na wanapenda sana lugha yetu ya Kiswahili
kwamba kumbe lugha ya Kiswahili ni nzuri kuliko hata lugha yao, wanasema lugha
yao ni ngumu kuliko kiswahili kwa vile ni rahisi sana.
“Sisi
kimetusaidia kuliko mataifa mengine tuliyonayo kama Bangladesh, ndugu zetu wa
Malawi au Afrika Kusini.
“Kwa hiyo
sisi wanatupenda sana hata maeneo tuliyopo sasa tunafanya kazi kwa karibu hapa
tulipo kwa vile tuko
karibu,
tukitoka tu nje tunakutana nao kwa hiyo Kiswahili kinasaidia sana."
Je raia
wanasemaje? Augustine ni mkazi wa Goma
jimboni Kivu Kaskazini na anakiri kuwa Kiswahili kinawaunganisha na Watanzania
akisema, "Kiswahili kinatusaidia sisi wanacongo na Watanzania.
“Ni lugha ya
dunia nzima na ndio maana nasema ni lugha ya amani Afrika Mashariki kwa vile
sisi sote tunaongea lugha moja.
“Mimi
nitachanganya na kifaransa watanzania wanasema wanaongea Kiswahili sanifu
lakini sisi sote tunaelewana katika mazungumzo yetu na kutafuta amani nchini
Congo.
“Kiswahili
kinaleta mahusiano kama niko hapa na mtu wa Bangladesh hawezi kunielewa lakini
mtu wa kutoka Afrika Mashariki tutaelewana kwa vile sote tunazungumza Kiswahili
na pia inaleta amani."