MHADHIRI Mwandamizi katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Dk Benson Banna, amesema adhabu iliyotolewa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Halima Mdee na Ester Bulaya ya kufungiwa shughuli za Bunge kwa
takriban mwaka mmoja ni sahihi.
Wabunge hao walipewa adhabu hiyo juzi
kwa kosa la utovu wa nidhamu katika kikao cha Bunge na kukidharau Kiti cha
Spika, Ijumaa iliyopita. Wabunge hao walionesha utovu huo wa nidhamu bungeni,
wakipinga Mbunge wa Kibamba, John Mnyika kutolewa nje ya Bunge kwa agizo la
Spika wa Bunge Job Ndugai.
Kutokana na Mnyika kukaidi amri ya
Spika ya kumtaka akae huku Mnyika akitaka ombi lake la utaratibu bila kujali
maelekezo ya Spika, Ndugai aliagiza askari kumtoa nje ya Bunge na kutohudhuria
vikao vya Bunge kwa wiki moja.
Wakati askari wakimtoa Mnyika
ukumbini, Halima ambaye ni mbunge wa Kawe na Bulaya wa Jimbo la Bunda Mjini,
waliinuka katika viti vyao na kuelekea upande wa askari waliokuwa wakimtoa nje
Mnyika huku Bulaya akihamasisha wabunge wengine wa upinzani kuondoka na kususa
Bunge.
Kutokana na hali hiyo, Ndugai
aliiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kujadili adhabu mwafaka
na ndipo baada ya mjadala, Bunge likaridhia wabunge hao kutoshiriki shughuli za
Bunge vikiwamo vikao vya Bunge na safari na vikao vya Kamati za Kudumu hadi
mwezi Aprili mwakani katika Bunge la Bajeti mwaka 2018/ 2019.
Akizungumza na gazeti hili, Dk Banna
alisema wabunge hao walidhalilisha Bunge, wapiga kura na wananchi katika
majimbo yao. Alisema wabunge wanapaswa kuheshimu kanuni za Bunge na kuzifuata
ili kufanya uwakilishi mzuri kwa wananchi.
“Kuna gharama ya kuwa Mheshimiwa na
hiyo ni kuwa na hekima kwa kuwa chochote kinyume na hapo ni kosa tena kubwa na
wabunge hao wamevuna kile walichokipanda,” alisema.
Mbunge wa Kaliua wa Chama cha
Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya alisema kuwa adhabu hiyo ni mwafaka kwa
wabunge hao kutokana na kuwa walikwishaonywa. Alisema, Bunge linatakiwa
kuheshimiwa na wabunge hao wamekuwa watata mara kwa mara katika kufuata kanuni
zilizowekwa.
Alisema, wabunge wanatakiwa kuwa na
nidhamu, uvumilivu na hekima ya hali ya juu kipindi chote wakati Bunge likiwa
linaendelea. Alisema kwa upande wa Mdee, ndani ya kipindi kifupi amefanya
makosa kadhaa ya utovu wa nidhamu.
Alisema, mbunge huyo aliitwa kwenye
kikao cha Kamati ya Nidhamu mwezi Aprili baada ya kudaiwa kumtukana Spika
Ndugai na alipewa karipio kali la kumtaka asirudie kosa. Alisema wakati wakiwa
kwenye kikao hicho, aliambiwa wazi kuwa iwapo atarudia tena kosa, atapewa
adhabu kali zaidi na kwa sasa anatumikia kile alichoonywa.
Kutetea wezi wa madini Wakati huo
huo, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde amesema kufukuzwa bungeni kwa wabunge
wa Upinzani, kumetokana na kutetea wezi wa madini kwani wamekuwa wakipinga
juhudi za Rais John Magufuli katika kuokoa rasilimali za Taifa yakiwamo madini.
Akizungumza kwenye Viwanja vya Bunge
jana, mbunge huyo wa CCM alisema, “Mimi ndio nilikuwa nachangia na hili jambo
la mchanga wa dhahabu lilikuwa linazungumziwa kipindi cha nyuma.
“Mwongozo wa Mnyika alisimama kama
anatetea wezi wa mchanga wa dhahabu watu wasifikiri kuwa kuna mtu ameonewa,
lakini hoja ya kutetea wezi wa dhahabu ndiyo imemgharimu Mnyika.”
Aliongeza Lusinde, “Tunajiuliza
maswali ni kwabnini watu hawa walikuwa wanapinga wizi kipindi cha nyuma, lakini
sasa wanatetea kuna nini kimetokea hapo katikati? “Kwa nini wanatetea wezi?
Rais John Magufuli amejitahidi kuokoa madini ili fedha zitusaidie katika huduma
zingine, lakini wabunge wanapinga.”
Naye Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato
Chumi (CCM) alisema, “Tulikuwa tunajadili mchanga wa dhahabu sasa tunapongeza
hatua alizochukua rais, lakini watu ambao walikuwa wanazungumzia suala hilo kwa
miaka mingi wanaanza kupinga, hapa lazima tuhisi kuwa kuna kitu huenda wamepewa
na hao wezi.”
Alieleza kuwa haiingii akilini kwa
wabunge ambao ni wazalendo kupinga juhudi zinazofanywa na Rais kama hawajapewa
fedha yoyote na hao waliokuwa wanaliibia taifa. “Ifike mahala tuseme ukweli
katika hili uzalendo ulitakiwa kwani tuliibiwa taifa na hiki ndicho kimefanya
Mnyika aadhibiwe kwa kuwa alitetea wezi na ndicho chanzo na mbunge mwingine
kuropoka kuwa ni mwizi kwa sababu haeleweki,” alieleza Chumi.
Alisema hata adhabu waliopewa wabunge
Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda Mjini), chanzo chake ni kumtetea John
Mnyika aliyekuwa anatetea wizi unaofanywa na kampuni za madini, jambo ambalo
halikubaliki na kuwaomba wabunge kuungana katika kushughulikia mambo ya
kitaifa.
Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM)
alisema wabunge hao wa Upinzani wanapaswa kuheshimu mamlaka inayoongoza Bunge.
“Waache waende. Pale bungeni kuna viongozi wetu, ni lazima kuwaheshimu.
Kuheshimu mamlaka ni muhimu na ni lazima,” alieleza Naibu Waziri huyo wa zamani.
Juzi, Bunge kwa pamoja, lilipitisha
adhabu ya kusimamishwa kwa mikutano mitatu wabunge wa Chadema, Mdee na Bulaya
kutokana na utovu wa nidhamu na kutoheshimu mamlaka ya Spika.
Hawatahudhuria mikutano ya Bunge
kuanzia juzi katika Mkutano wa Saba unaoendelea, Mkutano wa Nane mwezi Novemba
na ule wa Tisa Februari mwakani. Watarejea bungeni Aprili mwakani wakati wa
Mkutano wa Bunge la Bajeti, na muda wote huo hawataruhusiwa kushiriki shughuli
zozote za kibunge.
Kiini cha kufungiwa kwao ni vurugu
zilizotokea wakati Lusinde akichangia Bajeti ya Nishati na Madini, ambako
alikatizwa na Mnyika aliyekuwa akitaka Spika achukue hatua dhidi ya mbunge
aliyedai amemwita mwizi.
Katika hotuba yake ya Kambi ya
Upinzani kwa bajeti hiyo, Mnyika alipinga ripoti ya Kamati ya Rais Magufuli ya
uchunguzi wa makinikia, kiasi cha wabunge wengine kuhoji upinzani wana ajenda
gani na kueleza kuwa wanatumiwa na waliofilisi nchini katika sekta ya madini.