OKTOBA 10 dunia imeadhimisha siku ya afya ya akili ambayo huadhimishwa kila mwaka. Siku hii ambayo inatambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), kauli mbiu yake mwaka huu ni ‘afya ya akili mahala pa kazi’.
Katika mahojiano na mwandishi wa makala haya, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Msaikolojia Tiba Bingwa wa Afya ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Tasiana Njau anaeleza undani wa magonjwa ya akili na watu wanaoweza kuyapata. Njau anasema matatizo ya afya ya akili wakati mwingine yanaweza kuwa hayajafikia hatua ya kuwa ugonjwa.
Anasema katika sehemu za kazi, waajiri hawaoni kuwa matatizo ya afya ya akili yanaweza kumpata mfanyakazi yeyote na au pengine akahitaji tiba. Njau anasema kuna msongo ambao mtu anaupata mahala pa kazi kwa sababu mfanyakazi ni binadamu kama walivyo wengine.
“Binadamu haimaanishi akienda kazini ule utu wake ameufuta, anaenda kazini akiwa pengine ni mama au baba, ni mke au mume, ana marafiki, ana jamii yake ya familia ambavyo wakati mwingine vinaweza kumpa msongo… na kazi pia inaongeza baadhi ya msongo,” anasema Njau.
Njau anasema ama mzazi, kuna mambo yanayoweza kumsababisha msongo katika malezi na pia kuwa kwenye jamii kuna baadhi ya mambo yanayoweza kusababisha hali hiyo. “Kwa hiyo mara nyingi, maisha ya familia, ya kazi, kuwa na marafiki yote haya yanaweza kumshinda mtu kuyabeba yote na kujikuta anaegemea upande mmoja.
“Kuna mtu unakuta anakaa ofisini mpaka usiku anapitiliza muda wa kawaida na yuko peke yake au kazi anayotakiwa aifanye kwa nusu saa anaifanya kwa saa tatu. Hiyo inasababisha msongo wakati mwingine, hivyo utendaji kazi kupungua na ufanisi pia kupungua,” anasema Njau.
Anasema mtu huyo pamoja na kukaa kazini muda mrefu anaweza pia akaondoka kazini bila kumaliza kazi aliyokuwa akiifanya kwa sababu umakini wake kwenye kazi hiyo haukuwepo. Anasema kuna watu pia wanakunywa pombe kupita kiasi na asipokunywa, hawezi kufanya kazi.
Mambo kama haya yanapojitokeza miongoni mwa wafanyakazi, ni ishara kuwa mahala pa kazi kuna watu ambao wana matatizo ya afya ya akili. “Nikisema matatizo ya afya ya akili ni tofauti na kusema mtu kachanganyikiwa na siyo lazima mtu huyo awe ni mgonjwa wa magonjwa ya akili,” anasema Njau na kuongeza kuwa matatizo ya afya ya akili ni kama vile msongo.
Hata hivyo, Njau anasema kuna watu ambao katika maisha yao yote wanaishi na matatizo hayo. Anatoa mfano wa tatizo la hofu na wasiwasi ambalo ni miongoni mwa matatizo ya afya ya akili yanayopunguza utendaji wao wa kazi.
“Kwa mfano, mtu akiwa na hofu ya kuongea mbele za watu inaweza kumfanya utendaji wake wa kazi ukawa siyo mzuri kama kazi yake itahusisha kuzungumza na watu. Lakini ni tatizo anaishi nalo pengine miaka yote,” anasema Njau.
Njau anasema WHO imetamka kuwa ifikapo mwaka 2030 ugonjwa wa sonona ambao ni kati ya magonjwa zaidi ya 360 ya afya ya akili, utakuwa mkubwa. Ugonjwa huu husababisha udhaifu wa mtu katika kufanya kazi zake.
Ndiyo maana mwaka huu, ujumbe mkuu wa shirika hili la afya duniani umesimama katika ugonjwa huo. Anasema shirika hilo linatambua pia kuwa mtu mmoja kati ya wanne katika maisha yao kuna kipindi atapata magonjwa ya akili.
“Kuna watu wanasema mmoja kati ya watu wanne ni vichaa, hii siyo sahihi na sivyo inavyomaanisha. Ila tafiti zinavyofanyika zinafanyika kwa watu tofauti na siyo kuchukua watu wanne wa kundi moja… kwa mfano, isiwe kabila moja wote, isiwe jinsia moja, isiwe vijana wote,” anasema.
Anasema kuna vitu vingi vinaangaliwa katika kufanya utafiti. Anaiasa jamii kutopokea taarifa ambazo si sahihi. Anasema katika sehemu za kazi imeonesha kuwa kuna watu wengi ambao wana tatizo la sonona na imeonesha kuwa watu hawajali tatizo la afya ya akili katika sehemu za kazi.
“Kunakuwa na namna mbili ya kutokujali matatizo ya afya ya akili makazini,” anasema. Anafafanua kuwa, “mfanyakazi akiwa na msongo, akimwambia bosi wake leo nina msongo siwezi kuja kazini hawezi kukuelewa. Lakini akimwambia ana malaria au kifua kikuu anajali, na atakupa msaada.”
Njau anasema sehemu za kazi hakuna utaratibu mzuri wa kuhakikisha wafanyakazi wao wanaishi katika mazingira yanayowaweka mbali na matatizo ya afya ya akili. Aidha anasema afya nzuri ya akili inatengenezwa pia na mazingira bora ya kazi ambayo ni pamoja na kuandaa vitu vya kuwafanya wafanyakazi wafurahie kazi, kuwaburudisha na pia kufanya akili zao zipumue.
“Kuna vitu kama ‘family day’, vitu kama hivyo vilikuwa na nia ya kuondoa msongo kwa wafanyakazi kuwafanya wafurahi na kusahau kama kuna mambo mengine yanapita na kuanza upya, lakini ofisi nyingi siku hizi hawafanyi,” anasema Njau.
Njau anasema kampuni nyingi zimekuwa na visingizio mbalimbali vinavyofanya sherehe hizo zisifanyike. Miongoni mwake ni ufinyu wa bajeti. Anasema hata sherehe hizo zikifanyika, hazifanyiki kwa utaalamu ambao unafanya wafanyakazi wapate faida iliyokusudiwa.
Taasisi nyingine wakifanya sherehe hizo wanaandaa na mafunzo ya namna gani watumishi wanaweza kujilinda na tatizo la msongo jambo ambalo siyo sahihi kwani siku hiyo ni ya watu kupumzika.
Njau anasema pia mahitaji ya kuondoa msongo kwa wafanyakazi inategemea kulingana na muundo wa kazi na siyo lazima wafanyakazi wote washiriki sherehe hizo za familia. “Lakini ni vizuri kwamba katika taasisi na kampuni, kuwe na utaratibu kwamba vitu ambavyo vinasaidia kuondoa msongo na matatizo mengine ya afya ya akili iwe ni sehemu ya vitu muhimu,” anasema.
Njau anasema wataalamu wa afya ya akili wanashauri kila ofisi iwe na programu ya ustawi wa wafanyakazi ambayo itahusisha afya kwa ujumla; yaani ya kimwili na ya akili. Lakini ifahamike kuwa programu hiyo haifanani kati ya ofisi moja na nyingine, au taasisi moja na nyingine. Njau anasema inaweza ikatokea mfanyakazi amepata ugonjwa wa hofu na wasiwasi.
Kisha akapata tatizo la ghafla la moyo kwenda mbio sana. Lakini wafanyakazi hawatajua namna ya kumpa huduma ya kwanza na kumsaidia kwa sababu hawana mafunzo. Anasema kwa sababu ya matatizo mbalimbali ya afya ya akili yanasababisha utendaji kazi usio mzuri, ni vizuri kuwe na utaratibu mzuri wa kuwasaidia wafanyakazi