Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
amekutana na mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) huku
uchaguzi wa marudio ambao umekumbwa na utata ukiendelea kukaribia.
Mwenyekiti huyo wa tume alikuwa amekutana na mgombea wa upinzani Bw Raila Odinga Ijumaa.
Bw Odinga alijiondoa kutoka kwenye uchaguzi huo wa Alhamisi akisema hana imani uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki.
Uchaguzi huo wa 26 Oktoba unaandaliwa baada ya Mahakama ya Juu kufuta uchaguzi wa kwanza uliofanyika tarehe 8 Agosti ikisema kulikuwa na kasoro nyingi.
Bw Chebukati wiki iliyopita alikuwa ameitisha mkutano wa wagombea wote wa urais lakini baadaye akauahirisha na baadaye akakutana na Bw Odinga kivyake.
Alidokeza kwamba anapanga kuwakutanisha Bw Odinga na Bw Kenyatta baadaye baada kukutana na rais huyo.
Taarifa kutoka ikulu imesema Rais Kenyatta amemwambia mwenyekiti huyo kwamba yuko tayari kwa uchaguzi huo wa marudio na hana masharti yoyote kwa tume hiyo..