FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

WAMILIKI SHULE BINAFSI WAOMBA KUPATA MKOPO


SERIKALI imeombwa kuwasaidia wamiliki wa shule binafsi mkoani Dodoma ili waweze kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo mifuko ya hifadhi ili ziweze kuchukua wanafunzi wengi hasa katika kipindi hiki ambacho serikali imehamia mkoani hapa.
Pia wameiomba serikali kuwaingiza katika mgao wa kupata vitabu kama inavyofanya katika shule za serikali ili kuonesha mchango wao katika sekta ya elimu unathaminiwa na serikali. Maombi hayo yalitolewa juzi na Mkurugenzi wa Shule ya Msingi El Shaddai iliyopo mjini Dodoma, Juliana Assey wakati akimkaribisha mgeni rasmi katika mahafali ya nne ya darasa la saba aliyofanyika shuleni hapo juzi.
Alisema changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni uwezo mdogo walionao wa kuweza kufanya jambo kwa haraka ili waendane na kasi iliyopo ya serikali kuhamia Dodoma na hivyo kuiomba serikali kuwasaidia kupata mikopo hiyo.
“Serikali wakati mwingine imekuwa ikitumia mifuko ya hifadhi ya jamii kujenga taasisi zao wenyewe, hivyo sisi kama wamiliki wa shule binafsi tungependa utaratibu huo utumike pia kwetu kwa kutujengea majengo tunayotaka na tutalipa kwa kuwa mabenki hawataki kutukopesha kwa kutumia dhamana ya shule,” alisema mkurugenzi huyo. Akizungumzia kuhusu upewaji wa vitabu alisema kupitia utaratibu uliopo kwa serikali wa kutoa elimu bila ya malipo basi wanaomba iwafi kirie na shule binafsi kuwapa mgao wa vitabu.