KUENDELEA kusuasua kwa maendeleo na ufaulu katika masomo ya Hisabati na Sayansi, kumewafanya wadau mbalimbali kushirikiana na kutafuta namna ambavyo wanaweza kuongeza ufaulu katika masomo hayo.
Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu ya Halotel, wamekutana na kuja na mfumo ambao wanaona unaweza kuwa moja ya suluhisho katika kuongeza ufaulu. Mfumo huo wa kimtandao ambao unafuata mtaala wa kufundishia wa Tanzania na umepewa jina la Halostudy, uko katika majaribio na tayari umejaribiwa kwa Shule ya Sekondari ya Lugoba iliyoko Chalinze mkoani Pwani, kuona ni namna gani unaweza kuwa na manufaa kwa wanafunzi na walimu katika kujenga Tanzania ya viwanda.
Akizungumzia mfumo huo, Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Mtandao kutoka Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (CoICT) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Joel Mtebe alisema mfumo huo unaweza kuwa suluhisho kubwa katika kuongeza ufaulu kwa masomo ya sayansi na hisabati kwani unatumia njia za kisasa kutoa mafunzo. “Mfumo huu utawasaidia wanafunzi na walimu, wanafunzi wanaweza kujifunza masomo ya sayansi au hisabati popote pale walipo ili mradi wawe na simu au kompyuta iliyowezeshwa kuwa na intaneti.
Masomo ya sayansi na hisabati yanatumia njia tofauti za ufundishaji na mfumo huu umezingatia yote hayo kwa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, kila somo lina mchanganyiko wa sauti zilizorekodiwa, video pamoja na njia nyingine zinazomuwezesha mwanafunzi kujisomea mwenyewe,” alieleza Mtebe.
Aliongeza, “Mfumo huu, utamuwezesha mwanafunzi mfano anapotaka kujifunza jinsi moyo unavyofanya kazi ataweza kuona moja kwa moja kupitia video zenye mfano halisi namna moyo unavyofanya kazi katika mwili wa binadamu, tofauti na kuchorewa moyo ubaoni vilevile hata katika masomo ya kemia anapotaka kuchanganya kemikali na kuona jinsi rangi inavyoonekana, kwa ubaoni ni ngumu mno, lakini kwa mfumo huu mwanafunzi ataona moja kwa moja matokeo hata kama shule haina maabara.” Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Kampuni ya Halotel, Mhina Semwenda alisema kampuni hiyo imefurahi kuwa sehemu ya kuleta mabadiliko katika mfumo wa elimu ya Tanzania.