FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

Uhuru aelekea tena Ikulu


WAKATI Rais anayewania kurejea katika Ikulu ya Kenya, Uhuru Kenyatta (55) akionekana kuongoza kwa tofauti ya kura milioni 1.4 kufi kia jana jioni, mgombea urais kwa tiketi ya Muungano wa Vyama vya Upinzani (NASA), Raila Odinga (72) amedai kuwa, hatayakubali matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika juzi.
Amejenga hoja akidai kuwa, mfumo wa kielektroniki wa kupokea matokeo wa Tume ya Uchaguzi Isiyokuwa na Mipaka (IEBC) umefanyiwa udukuzi. Raila, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, amedai matokeo ya awali ya uchaguzi yanayoendelea kutangazwa ni matokeo ya udukuzi, uliofanywa katika kanzidata ya IEBC na kwamba hayajaambatanishwa na Fomu 34A kama sheria ya uchaguzi inavyotaka. Hata hivyo, Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati amesema ana uhakika mfumo wa taasisi hiyo hauna dosari.
Lakini alisisitiza madai hayo yanafanyiwa kazi kuona kama kuna mfumo umefanyiwa udukuzi.Aidha, ameagiza fomu 34A na 34B zihakikiwe kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya kiti cha urais chenye wagombea wanane, lakini wanaopewa uzito zaidi wakiwa Raila na Uhuru anayewania tena kuiongoza Kenya baada ya kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2013. Raila, akizungumza jana katika mkutano na wanahabari, alisema; “Kinachotumwa IEBC ni vitu vya kughushi kabisa… vinalenga kumpa ushindi Uhuru Kenyatta kura ambazo hazikupigwa …tumegundua ujanja wao.
Watu wanapaswa kuwajibika,” alisema Raila katika mkutano na wanahabari. Alisisitiza kuwa, matokeo yaliyotumwa kutoka katika majimbo mbalimbali, hayana uwiano na yale yanayojumlishwa katika kituo kikuu cha kujumulishia cha Bomas, jijini Nairobi. “Udanganyifu huu unafanyika ndani ya saa 12 za kazi nzuri ya kidemokrasia katika sanduku la kura, si sawa, haki itendeke.
Kimsingi, tunawaambia watu wetu wasikubali matokeo haya, ila wawe watulivu…,” aliongeza mgombea mwenza wa Raila, Kalonzo Musyoka. Hata hivyo, Raila hakueleza chanzo cha taarifa za kuwapo kwa udukuzi, zaidi ya kudai anahusisha na kifo cha ofisa wa IEBC, Chris Msando aliyekuwa Meneja wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa IEBC. Alidai kuwa, tayari alishaandaa hotuba yake ya ushindi, na si vinginevyo huku akisisitiza kuwa, alishindwa urais katika uchaguzi mmoja tu, alioshiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1997.
“Lakini mwaka 2007 na 2013 nilinyimwa ushindi kwa hila, ila kwa mwaka huu ninaamini ushindi ni wangu, ndiyo maana nikaandaa hotuba moja tu, sasa haya mambo mengine yanayoanza kwa kweli sitawaelewa,” alisema na kuwataka wafuasi wake wawe na subira. Mmoja aitema Ikulu Wakati Raila akilalamikia matokeo, mmoja wa wagombea urais, Dk Japheth Kayulu aliyewania uraia akiwa mgombea huru, amekubali kushindwa. Dk Kayulu ambaye kufikia jana mchana alikuwa amejikusanyia kura 36,451, amekubali kushindwa akiwa anashika nafasi ya sita kati ya wagombea wanane.
Wakati anatangaza hayo, Uhuru Kenyatta alikuwa anaendelea kuongoza kwa kura 7,930,242 akifuatiwa na Raila (6,529,158), Joseph Nyaga (36,451), Mohammed Abduba Dida (34,832) na Ekuru Aukot (26,107) akishika nafasi ya tano. Nafasi ya saba ilishikwa na Shakhalaga Cyrus Jirongo (10,890) na Michael Wainanina Waura alikuwa na kura 8,582 zilizomweka katika nafasi ya nane.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2013, Uhuru alishinda kwa kura 6,173,433 sawa na asilimia 50.51 dhidi ya kura 5,340,546 za Raila, sawa na asilimia 43.7, ikiwa ni tofauti ya kura 832,887. Waliojiandikisha kupiga kura walikuwa milioni 14.3. Matokeo yafutwa Katika hatua nyingine, IEBC imefuta matokeo ya Jimbo la uchaguzi la Kilgoris, baada ya idadi ya kura kuzidi idadi ya wapigakura waliokuwa wameandikishwa.
Msimamizi wa Jimbo hilo, Elijah Ombogo alisema idadi ya wapigakura walioandikishwa ilikuwa 285, lakini kura zilizopigwa ni 325, jambo lililomlazimu kuyafuta matokeo, huku akiwataka wasimamizi wa vituo kujieleza. Auawa kituoni Katika Jimbo la Mugirango Kusini, mtu mmoja ameuawa na askari Polisi katika kituo cha kukusanyia kura katika Kaunti ya Kisii, baada ya kudaiwa kutotii amri ya kukaa mbali na eneo hilo.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mtu huyo aliuawa kwa kipigwa risasi mgongoni wakati akiamulia ugomvi wa wakazi wawili katika eneo la kituo cha Shule ya Sekondari ya Wasichana na Nduru. Raila ang’ara gerezani IEBC ilitangaza kuwa kwa kura zilizopigwa na wafungwa, Raila Odinga aling’ara kwa kupata kura 2,048, Uhuru (1,710), Nyagah (9), Dida (7), Aukot (4), Jirongo (2), Japhet Kaluyu (2) na Waura (2).
Nje ya Kenya Aidha, kwa kura zilizopigwa nje ya Kenya, kwa upande wa vituo vilivyotumika nchini Tanzania, Uhuru alipata kura 393, akizidiwa kwa kura moja na Raila aliyepata kura 394. Aukot (2), Dida (2), Waura (1) na wagombea wengine hawakupata kura. Katika vituo vya nchini Burundi, Uhuru alipata kura 47, huku Raila akipata kura 48, Waura (1) na wengine hawakupata kura.
Nchini Rwanda, Uhuru amepata kura 298, Raila (255), Nyagah (1) na wengine hawakupata kura. Huko Afrika Kusini, Uhuru amepata kura 358, Raila (302), Aukot (4), Waura (2), Nyagah (1) na wengine hawakupata kura. Nchini Uganda, Uhuru amepata kura 408, Raila (322), Aukot (2), Dida (3) na wengine hawakupata kura. Mshauri wa Raila atoroka Habari zaidi zinasema Mshauri wa mgombea urais kwa tiketi ya Nasa, Salim Lone amelazimika kukimbilia Marekani, akidai kutishiwa maisha nchini Kenya.
Lone amekimbilia New York, Marekani akidai kuwa watu waliomtesa na kumuua Meneja wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa IEBC, Chris Msando, wamemtishia maisha. Alikaririwa na gazeti la Kenya la The Standard, akisema kuwa pamoja na kulazimika kutoroka ghafla, hilo halijaathiri mawasiliano yake na muungano huo wa vyama vya upinzani.
“Sikuwa na jinsi zaidi ya kusalimisha maisha yangu kwa sababu nimetishiwa. Hata hivyo, ninashiriki katika kampeni kwa asilimia mia moja,” alikaririwa akisema na kuongeza kuwa, atarejea Kenya endapo Raila ataibuka mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Watumia mitandao waonywa Kaimu Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Kenya, Fred Matiang’i aliwaonya watumiaji wa mitandao ya kijamii kuwa makini na taarifa za uchochezi, zinazosambazwa na kwamba watakaobainika kuhusika katika uchochezo watachukuliwa hatua za kisheria.
Mikakati ya Uhuru Jana jioni, Katibu Mkuu wa chama tawala cha Jubilee, Raphael Tuju aliweka hadharani mikakati ya Uhuru, akisema endapo atafanikiwa kurejea madarakani, atajadiliana na wapinzani ili kuangalia namna ya kushirikiana katika kuijenga nchi yao.
“Tunasubiri matokeo, kama yakiwa mazuri kwa upande wetu, kitu cha kwanza ni kuwafikia wenzetu wa NASA ili kujenga mshikamano utakaosukuma mbele maendeleo ya nchi yetu,” alisema. Awali, Tuju aliwataka wapinzani kuwa tayari kwa matokeo yoyote endapo Rais Kenyatta atatangazwa kutetea nafasi yake. Hata hivyo, awali, Raila ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, alisisitiza kutoyatambua matokeo akidai umefanyika udukuzi katika nafasi zote sita ndani ya kaunti 47