KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, imefi kia lengo la kuuza hisa zake 560,000,000 zenye thamani ya Sh bilioni 476 kama ilivyokuwa imepangwa.
Katika mauzo hayo yaliyoanza
Machi 9, mwaka huu na kuhitimishwa Julai 28, mwaka huu ambapo kila hisa iliuzwa
kwa Sh 850, mauzo ya asilimia 60 yamehusisha wawekezaji wa ndani wakati
asilimia 40 imehusisha wawekezaji wa kigeni Kwa mujibu wa taarifa ya Vodacom
kwa vyombo vya habari, taarifa ya mauzo ya hisa inazingatia idhini ya Mamlaka
ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kuhusu toleo hili la Hisa, na kwamba
wawekezaji ambao maombi yao yamekubaliwa wataingiziwa hisa zao katika akaunti
zao zinazohifadhiwa na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Stakabadhi za Umiliki wa Hisa
zinaweza kupatikana kutoka kwa mawakala ambako hisa husika zilinunuliwa. Toleo la
Hisa za Vodacom Tanzania limekuwa toleo kubwa zaidi na la kihistoria kufanyika
nchini, na kuhusisha Watanzania zaidi ya 40,000 wengi wao wakiwa wanashiriki
kwa mara ya kwanza katika masoko ya mitaji hapa nchini.
“Kwa hiyo, Toleo hili
limewezesha kupanuka kwa ushiriki wa wananchi katika soko la mitaji na dhamana,
na pia katika uchumi wa Taifa,” ilisema sehemu taarifa hiyo. Hisa hizo
zitaorodheshwa DSE na mauzo yake kuanza Agosti 15, mwaka huu. Kutokana na
kukamilika kwa uuzaji huo wa hisa, Vodacom imeelezea kufurahishwa na
kuwashukuru Watanzania kwa uamuzi wa kuiunga mkono kampuni hiyo.