FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

Mjadala wa bajeti kutikisa bunge siku 7




BAADA ya maoni ya wasomi, wanasiasa, taasisi kadhaa na wananchi wa kawaida, mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 unahamia bungeni.
Kuanzia leo kwa siku saba hadi Juni 20, mwaka huu, wabunge watajadili kabla ya kuamua kwa kura ya wazi kupitisha Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 iliyowasilishwa bungeni Alhamisi iliyopita. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliwasilisha bungeni Bajeti ya Serikali yenye thamani ya Sh trilioni 31.7 zinazotarajiwa kukusanywa na kutumika kuanzia Julai mosi, 2017 hadi Juni 30, 2018.
Dk Mpango alisema jumla ya mapato ya ndani, yakijumuisha mapato ya halmashauri, yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 19.977.0, sawa na asilimia 63.0 ya bajeti yote. “Kati ya mapato hayo, serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya shilingi bilioni 17,106.3 sawa na asilimia 85.6 ya mapato ya ndani. “Aidha, mapato yasiyo ya kodi ni shilingi bilioni 2,183.4 na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni shilingi bilioni 687.3,” alieleza Dk Mpango.
Alisema Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 3.971.1 ambayo ni asilimia 12.5 ya bajeti yote, ambayo imepokewa kwa pongezi nyingi na wasomi, wachumi, wananchi wa kawaida na wanasiasa mbalimbali waliotoa maoni yao baada ya kuwasilishwa. Miongoni mwa mambo yaliyowafurahisha wengi katika bajeti hiyo ni kufutwa ada ya kila mwaka ya leseni ya magari; kufuta ada ya ukaguzi wa viwango vya mazao ya biashara; kutoza kodi ya VAT kwa kiwango cha sifuri kwa huduma zinazotolewa kwenye usafirishaji wa bidhaa/mizigo nje ya nchi.
Pia kuwatambua rasmi wafanyabiashara wadogo wasio rasmi kama machinga, mama lishe, wauza mitumba; kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwenye malighafi na vifaa vinavyoagizwa nje kwa ajili ya kuunganisha na kutengeneza vifaa ambavyo ni mahsusi kwa ajili ya matumuzi ya walemavu. Pia kutoa msamaha wa kodi, riba na adhabu zinazoambatana na madeni yote (Tax Amnesty) ya ada ya leseni ya magari, ni eneo jingine lililowafurahisha wananchi wengi pamoja na wabunge.
Kupigwa marufuku kwa kusafirishwa kwa madini kutoka mgodini hadi moja kwa moja nje ya nchi, pia ni eneo jingine lililowagusa watu wengi hasa wakati huu ambao imebainika kuwa rasilimali ya madini inaibwa kwa kiasi kikubwa na wawekezaji wa migodi nchini. Mambo mengine mazuri ya bajeti ni kuondolewa kwa kodi katika masuala ya mafuta ya kula, vyakula vya mifugo na mbolea, na hivyo kuleta unafuu mkubwa kwa wakulima na wafugaji pamoja na Watanzania wanaoendesha viwanda vya kusindika mafuta ya kula.
Wabunge wengi hasa wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walionesha kufurahishwa na bajeti hiyo wakati ikisomwa na Dk Mpango. Mara kadhaa walimfanya asite kuendelea kuisoma kutokana na kumkatisha kwa nderemo na vifijo na wengine wakirukaruka walipokaa na kupiga meza kuonesha bajeti imekata kiu yao. Hata Spika wa Bunge, Job Ndugai alifikia mahali akasema ni vyema angewahoji wabunge kama waziri asiendelee kuisoma maana bajeti hiyo imejibu kila kitu. Baada ya Dk Mpango kumaliza saa 2.09 za kuisoma bajeti hiyo ya pili ya uongozi wa Rais John Magufuli, Spika Ndugai alikazia kwa kusema, “Haijapata kutokea.”
Kwa hiyo, kwa siku saba kuanzia leo, wabunge watapata fursa ya kukazia kile walichokuwa wakikifurahia bungeni wakati bajeti ilipokuwa inawasilishwa kwao. Matarajio ya wengi ni kwamba mjadala hautakuwa mkali sana, ingawa yapo maeneo wabunge wanaweza kuishauri serikali kuendelea kuyaboresha kwa nia ya kuwapa unafuu wananchi wanyonge ambao Rais Magufuli amejitanabaisha kuwa anakusudia kuwakomboa. Kwa mujibu wa Spika Ndugai, mjadala wa leo utaanza kwa kupokea maoni ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia ambaye ni Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM).
Kamati hiyo kwa takriban siku tano ilifanya mashauriano na serikali kuhusu mwelekeo wa bajeti hiyo baada ya wabunge kumaliza kujadili na kupitisha bajeti za kisekta. Akimaliza mwenyekiti huyo wa Bajeti, itakuwa zamu ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwasilisha maoni yake kabla ya wabunge wengine kutoa maoni yao. Wakati huo huo, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TSPF), imeipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwasilisha bajeti nzuri bungeni wiki iliyopita. Akizungumza katika Kongamano la Pili la Uwezeshaji mjini hapa juzi, Mkurugenzi wa Sera, Utafiti na Uwezeshaji wa TSPF, Gili Teri alisema bajeti ina mambo mengi mazuri.
Aliyataja baadhi ya mambo hayo ni kupunguzwa kwa kiwango cha Kodi ya Mapato ya Makampuni kutoka asilimia 30 hadi 10 kwa miaka mitano kuanzia mwaka mwekezaji atakapoanza uzalishaji. Teri alisema hali hiyo itasaidia sana katika ushindani kwenye uwekezaji hasa kwa wawekezaji wa viwandani. Alieleza uzuri mwingine wa bajeti hiyo ni kwenye kodi zilizoondolewa katika mafuta ya kula, mbolea na vyakula vya mifugo, kwamba itawasaidia Watanzania katika kushiriki kwenye uchumi wa viwanda. Upinzani wadai bajeti ina mapungufu Kambi ya upinzani imesema jana kuwa bajeti ya mwaka huu ina mapungufu mengi na makubwa na imelenga kumnyonya mwananchi maskini.
Hotuba ya Upinzani inatarajiwa kuwasilishwa na Mbunge wa Mbozi, Joseph Silinde badala ya Waziri kivuli wa Fedha na Mipango, Halima Mdee ambaye amefungiwa kutohudhuria shughuli za kibunge kwa mikutano mitatu ya bunge. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Mdee alisema bajeti hiyo ina mapungufu mengi na makubwa na maoni ya kambi hiyo yatawasilishwa kwenye kitabu chenye kurasa 200.
Alisema baada ya kufanyika uchambuzi wa kina wa bajeti, iliyowasilishwa na kugundua mapungufu kadhaa ikiwemo kwani bajeti hiyo ambayo takwimu za vitabu vyake vya mapato na matumizi (Volume 1,11,111 na 1V) zinatofautiana sana, pia sura ya bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango inatofautiana pia na vitabu hivyo. Mdee alisema kitabu cha mapato ya serikali, kinaonesha kuwa serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ilikusanya jumla ya Sh trilioni 23.9, kitabu cha matumizi ya serikali kinaonesha kuwa serikali inakusudia kutumia jumla ya Sh trilioni 26.9 ikiwa ni ongezeko la matumizi ya Sh trilioni tatu ambayo vyanzo vyake havikuoneshwa kwenye kitabu cha mapato.
“Wakati huo huo sura ya bajeti iliyosomwa na waziri wa fedha inaonesha bajeti ya serikali kwa maana ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2017/2018 ni kiasi cha Sh trilioni 31.7 kiasi ambacho hakionekani popote kwenye mapato na matumizi ya serikali. Pia alisema kwa mujibu wa mpango wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano tarakimu ya Sh trilioni 31.7 inaonekana kwamba ni makisio ya bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2018/2019. Alisema mambo kama hayo yanaonesha mkanganyiko katika bajeti hiyo.
“Hii ni bajeti ambayo imedhamiria kuua kabisa dhana ya ugatuaji madaraka kwa serikali za mitaa kwa kuziondolea serikali za mitaa madaraka yake ya kisheria ya kukusanya kodi ya majengo, kodi ya mabango na ushuru wa huduma mijini kwa malengo ya kujiendesha na kurudisha madaraka hayo ya ukusanyaji kodi hizo serikali kuu kupitia TRA,” alisema. Mdee alisema hiyo ni bajeti ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, inawalipisha Watanzania maskini wasio na uwezo wa kumiliki magari kodi ya ada ya mwaka ya leseni za magari kwa kuihamishia kodi hiyo kwenye ushuru wa bidhaa za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa ambapo athari zake ni kupanda kwa nauli katika sekta ya usafirishaji.
Alisema jambo hilo litasababisha kupanda kwa bei za vyakula, kupanda kwa bei za kusaga na kukoboa nafaka kwa kutumia mashine zinazotumia petrol na dizeli kwa wananchi waishio vijijini. Pia alisema kuwa wananchi maskini watapata changamoto kwani wengi wanatumia mafuta ya taa kwa ajili ya kupikia na matumizi mengine ya nyumbani. Pia alisema bajeti hiyo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania serikali itatoza kodi ya Sh 10,000 kwa nyumba zote katika halmashauri zote nchini zikiwemo nyumba za tembe na tope.
“Hii ni bajeti ambayo imeendelea kupandisha kodi kwenye bidhaa ambazo uzalishaji hutumia malighafi inayozalishwa ndani ya nchi. Alisema kambi rasmi ya upinzani bungeni itatoa vipaumbele katika sekta ya elimu ambayo itatengewa asilimia 20 ya bajeti ya maendeleo, sekta ya viwanda itatengewa asilimia 15, sekta ya nishati asilimia 15, sekta ya kilimo asilimia 10 na sekta nyingizo zitapata asilimia 40 iliyobaki bajeti ya maendeleo. Alisema vipaumbele hivyo vikitekelezwa kwa ukamilifu Tanzania itapunguza umaskini kwa asilimia 50 kwa kuwa ni vipaumbele vitakavyochochea ajira kwa watu wengi.