FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

Stars yaanza kwa sare







TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars jana ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Lesotho katika mechi ya kuwania kufuzu michuano ya kombe la mataifa Afrika ‘Afcon’ 2019 kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Matokeo hayo hayaiweki Stars kwenye nafasi nzuri sana ya kusonga mbele kwenye michuano ambayo mshindi wa kila kundi ndiye atakayefuzu moja kwa moja fainali. Tanzania na Lesotho zipo kundi A pamoja na timu za Uganda na Cape Verde zinazotarajiwa kucheza leo.
Nahodha Mbwana Samatta ndiye aliyeanza kuwainua watanzania vitini kwa kuandika bao la kuongoza kwa mpira faulo uliokwenda moja kwa moja nyavuni katika dakika ya 27. Mwamuzi aliamuru faulo hiyo ipigwe baada ya beki wa Stars Gadiel Michael kuchezewa vibaya na beki wa Lesotho.
Dakika saba baadae wageni Lesotho walisawazisha bao hilo kupitia kwa Thapelo Tale aliyeunganisha pasi nzuri ya Jane Thaba- Ntso na kuujaza mpira wavuni. Katika kipindi cha kwanza timu hizo zilishambuliana kwa zamu ingawa dakika za mwanzoni Stars ilikosa mabao kadhaa Samatta, Thomas Ulimwengu na Shizza Kichuya.
Stars iliendelea na mashambulizi yake mpaka katika kipindi cha pili lakini kutokuwa makini kwa safu yake ya ushambuliaji kuliwakosesha mabao mengi. Katika mechi nyingine zilizochezwa jana, kundi B Malawi iliifunga Comoro bao 1-0 na wenyeji wa michuano hiyo ya 2019 Cameroon wakiwapata matokeo kama hayo dhidi ya Morocco.
Kundi C Burundi ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Sudan Kusini huku Nigeria ilifungwa mabao 2-0 na Afrika Kusini nyumbani katika kundi E na kundi F Sierre Leone ikiifunga Kenya mabao 2-1.
Kundi I Botswana ikiwa nyumbani imefungwa bao 1-0 na Mauritania huku kundi K Zambia ikiwa nyumbani nayo ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Msumbiji na Guinea Bissau ikiifunga Namibia bao 1-0. Mechi hiyo ni ya tatu kwa Stars kucheza chini ya kocha Salum Mayanga baada ya kushinda mabao 2-1 dhidi ya Burundi na 2-0 dhidi ya Botswana katika mechi za kirafiki za kimataifa Machi mwaka huu.