FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM
Showing posts with label kitaifa. Show all posts
Showing posts with label kitaifa. Show all posts
MZAZI ATUPWA JELA MIKA 30 KWA KUZAA NA BINTI YAKE

MZAZI ATUPWA JELA MIKA 30 KWA KUZAA NA BINTI YAKE



Mahakama ya wilaya ya Misungwi jijini Mwanza imemuhukumu baba mmoja kwenda jela kutokana na kukutwa na hatia ya kumzalisha mtoto wake wa kumzaa.

Mzazi huyo, Jacob Shabani (30) mkazi wa Kijiji cha Wanzamiso, Misungwi alihukumiwa kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kufanya mapenzi na mwanaye wa kuzaa akiwa na umri wa miaka 14.

Akitoa ushahidi wake mahakamani hapo mtoto huyo alisema “Baba alinipa ujauzito mara tatu, nilizaa mara mbili mtoto mkubwa alifariki mwaka jana kesi ilipokuwa imeanza, mimba moja iliharibika baada ya kunipiga sana, na sasa nina mtoto mdogo ana mwaka mmoja.”.

Mtoto huyo amesema hali hiyo ilitokea baada ya baba yake kutengana na mama yake kuondoka nyumbani wakati yeye akiwa na miaka 12 mwaka 2015 na ndipo baba yake aliza kufanya naye mapenzi.

Kwa upande mwingine, mzazi huyo ameiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu hiyo akidai kuwa yeye ni mzazi na anafamilia inamtegemea

Mjadala wa bajeti kutikisa bunge siku 7




BAADA ya maoni ya wasomi, wanasiasa, taasisi kadhaa na wananchi wa kawaida, mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 unahamia bungeni.
Kuanzia leo kwa siku saba hadi Juni 20, mwaka huu, wabunge watajadili kabla ya kuamua kwa kura ya wazi kupitisha Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 iliyowasilishwa bungeni Alhamisi iliyopita. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliwasilisha bungeni Bajeti ya Serikali yenye thamani ya Sh trilioni 31.7 zinazotarajiwa kukusanywa na kutumika kuanzia Julai mosi, 2017 hadi Juni 30, 2018.
Dk Mpango alisema jumla ya mapato ya ndani, yakijumuisha mapato ya halmashauri, yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 19.977.0, sawa na asilimia 63.0 ya bajeti yote. “Kati ya mapato hayo, serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya shilingi bilioni 17,106.3 sawa na asilimia 85.6 ya mapato ya ndani. “Aidha, mapato yasiyo ya kodi ni shilingi bilioni 2,183.4 na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni shilingi bilioni 687.3,” alieleza Dk Mpango.
Alisema Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 3.971.1 ambayo ni asilimia 12.5 ya bajeti yote, ambayo imepokewa kwa pongezi nyingi na wasomi, wachumi, wananchi wa kawaida na wanasiasa mbalimbali waliotoa maoni yao baada ya kuwasilishwa. Miongoni mwa mambo yaliyowafurahisha wengi katika bajeti hiyo ni kufutwa ada ya kila mwaka ya leseni ya magari; kufuta ada ya ukaguzi wa viwango vya mazao ya biashara; kutoza kodi ya VAT kwa kiwango cha sifuri kwa huduma zinazotolewa kwenye usafirishaji wa bidhaa/mizigo nje ya nchi.
Pia kuwatambua rasmi wafanyabiashara wadogo wasio rasmi kama machinga, mama lishe, wauza mitumba; kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwenye malighafi na vifaa vinavyoagizwa nje kwa ajili ya kuunganisha na kutengeneza vifaa ambavyo ni mahsusi kwa ajili ya matumuzi ya walemavu. Pia kutoa msamaha wa kodi, riba na adhabu zinazoambatana na madeni yote (Tax Amnesty) ya ada ya leseni ya magari, ni eneo jingine lililowafurahisha wananchi wengi pamoja na wabunge.
Kupigwa marufuku kwa kusafirishwa kwa madini kutoka mgodini hadi moja kwa moja nje ya nchi, pia ni eneo jingine lililowagusa watu wengi hasa wakati huu ambao imebainika kuwa rasilimali ya madini inaibwa kwa kiasi kikubwa na wawekezaji wa migodi nchini. Mambo mengine mazuri ya bajeti ni kuondolewa kwa kodi katika masuala ya mafuta ya kula, vyakula vya mifugo na mbolea, na hivyo kuleta unafuu mkubwa kwa wakulima na wafugaji pamoja na Watanzania wanaoendesha viwanda vya kusindika mafuta ya kula.
Wabunge wengi hasa wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walionesha kufurahishwa na bajeti hiyo wakati ikisomwa na Dk Mpango. Mara kadhaa walimfanya asite kuendelea kuisoma kutokana na kumkatisha kwa nderemo na vifijo na wengine wakirukaruka walipokaa na kupiga meza kuonesha bajeti imekata kiu yao. Hata Spika wa Bunge, Job Ndugai alifikia mahali akasema ni vyema angewahoji wabunge kama waziri asiendelee kuisoma maana bajeti hiyo imejibu kila kitu. Baada ya Dk Mpango kumaliza saa 2.09 za kuisoma bajeti hiyo ya pili ya uongozi wa Rais John Magufuli, Spika Ndugai alikazia kwa kusema, “Haijapata kutokea.”
Kwa hiyo, kwa siku saba kuanzia leo, wabunge watapata fursa ya kukazia kile walichokuwa wakikifurahia bungeni wakati bajeti ilipokuwa inawasilishwa kwao. Matarajio ya wengi ni kwamba mjadala hautakuwa mkali sana, ingawa yapo maeneo wabunge wanaweza kuishauri serikali kuendelea kuyaboresha kwa nia ya kuwapa unafuu wananchi wanyonge ambao Rais Magufuli amejitanabaisha kuwa anakusudia kuwakomboa. Kwa mujibu wa Spika Ndugai, mjadala wa leo utaanza kwa kupokea maoni ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia ambaye ni Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM).
Kamati hiyo kwa takriban siku tano ilifanya mashauriano na serikali kuhusu mwelekeo wa bajeti hiyo baada ya wabunge kumaliza kujadili na kupitisha bajeti za kisekta. Akimaliza mwenyekiti huyo wa Bajeti, itakuwa zamu ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwasilisha maoni yake kabla ya wabunge wengine kutoa maoni yao. Wakati huo huo, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TSPF), imeipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwasilisha bajeti nzuri bungeni wiki iliyopita. Akizungumza katika Kongamano la Pili la Uwezeshaji mjini hapa juzi, Mkurugenzi wa Sera, Utafiti na Uwezeshaji wa TSPF, Gili Teri alisema bajeti ina mambo mengi mazuri.
Aliyataja baadhi ya mambo hayo ni kupunguzwa kwa kiwango cha Kodi ya Mapato ya Makampuni kutoka asilimia 30 hadi 10 kwa miaka mitano kuanzia mwaka mwekezaji atakapoanza uzalishaji. Teri alisema hali hiyo itasaidia sana katika ushindani kwenye uwekezaji hasa kwa wawekezaji wa viwandani. Alieleza uzuri mwingine wa bajeti hiyo ni kwenye kodi zilizoondolewa katika mafuta ya kula, mbolea na vyakula vya mifugo, kwamba itawasaidia Watanzania katika kushiriki kwenye uchumi wa viwanda. Upinzani wadai bajeti ina mapungufu Kambi ya upinzani imesema jana kuwa bajeti ya mwaka huu ina mapungufu mengi na makubwa na imelenga kumnyonya mwananchi maskini.
Hotuba ya Upinzani inatarajiwa kuwasilishwa na Mbunge wa Mbozi, Joseph Silinde badala ya Waziri kivuli wa Fedha na Mipango, Halima Mdee ambaye amefungiwa kutohudhuria shughuli za kibunge kwa mikutano mitatu ya bunge. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Mdee alisema bajeti hiyo ina mapungufu mengi na makubwa na maoni ya kambi hiyo yatawasilishwa kwenye kitabu chenye kurasa 200.
Alisema baada ya kufanyika uchambuzi wa kina wa bajeti, iliyowasilishwa na kugundua mapungufu kadhaa ikiwemo kwani bajeti hiyo ambayo takwimu za vitabu vyake vya mapato na matumizi (Volume 1,11,111 na 1V) zinatofautiana sana, pia sura ya bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango inatofautiana pia na vitabu hivyo. Mdee alisema kitabu cha mapato ya serikali, kinaonesha kuwa serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ilikusanya jumla ya Sh trilioni 23.9, kitabu cha matumizi ya serikali kinaonesha kuwa serikali inakusudia kutumia jumla ya Sh trilioni 26.9 ikiwa ni ongezeko la matumizi ya Sh trilioni tatu ambayo vyanzo vyake havikuoneshwa kwenye kitabu cha mapato.
“Wakati huo huo sura ya bajeti iliyosomwa na waziri wa fedha inaonesha bajeti ya serikali kwa maana ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2017/2018 ni kiasi cha Sh trilioni 31.7 kiasi ambacho hakionekani popote kwenye mapato na matumizi ya serikali. Pia alisema kwa mujibu wa mpango wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano tarakimu ya Sh trilioni 31.7 inaonekana kwamba ni makisio ya bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2018/2019. Alisema mambo kama hayo yanaonesha mkanganyiko katika bajeti hiyo.
“Hii ni bajeti ambayo imedhamiria kuua kabisa dhana ya ugatuaji madaraka kwa serikali za mitaa kwa kuziondolea serikali za mitaa madaraka yake ya kisheria ya kukusanya kodi ya majengo, kodi ya mabango na ushuru wa huduma mijini kwa malengo ya kujiendesha na kurudisha madaraka hayo ya ukusanyaji kodi hizo serikali kuu kupitia TRA,” alisema. Mdee alisema hiyo ni bajeti ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, inawalipisha Watanzania maskini wasio na uwezo wa kumiliki magari kodi ya ada ya mwaka ya leseni za magari kwa kuihamishia kodi hiyo kwenye ushuru wa bidhaa za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa ambapo athari zake ni kupanda kwa nauli katika sekta ya usafirishaji.
Alisema jambo hilo litasababisha kupanda kwa bei za vyakula, kupanda kwa bei za kusaga na kukoboa nafaka kwa kutumia mashine zinazotumia petrol na dizeli kwa wananchi waishio vijijini. Pia alisema kuwa wananchi maskini watapata changamoto kwani wengi wanatumia mafuta ya taa kwa ajili ya kupikia na matumizi mengine ya nyumbani. Pia alisema bajeti hiyo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania serikali itatoza kodi ya Sh 10,000 kwa nyumba zote katika halmashauri zote nchini zikiwemo nyumba za tembe na tope.
“Hii ni bajeti ambayo imeendelea kupandisha kodi kwenye bidhaa ambazo uzalishaji hutumia malighafi inayozalishwa ndani ya nchi. Alisema kambi rasmi ya upinzani bungeni itatoa vipaumbele katika sekta ya elimu ambayo itatengewa asilimia 20 ya bajeti ya maendeleo, sekta ya viwanda itatengewa asilimia 15, sekta ya nishati asilimia 15, sekta ya kilimo asilimia 10 na sekta nyingizo zitapata asilimia 40 iliyobaki bajeti ya maendeleo. Alisema vipaumbele hivyo vikitekelezwa kwa ukamilifu Tanzania itapunguza umaskini kwa asilimia 50 kwa kuwa ni vipaumbele vitakavyochochea ajira kwa watu wengi.

Magufuli: Hakuna mchanga wa madini utakaotoka kwenda nje ya nchi







RAIS John Magufuli amesema kwa sasa hakuna mchanga wa madini utakaotoka kwenda nje ya nchi huku akiitaka kampuni ya uchimbaji madini nchini Acacia kutubu na kukubali makosa yake kama inataka kuendelea kufanya biashara nchini.
Ameagiza mamlaka zinazohusika kuiita kampuni hiyo na kabla ya jambo lolote inapaswa kuilipa serikali fedha kwa kuwa imefanya udanganyifu kwa muda mrefu, wakishakubali hayo tunaweza kukaa kwa makubaliano. Ametoa kauli hiyo baada ya kupokea ripoti ya kamati ya pili iliyoundwa kuchunguza mchanga wa madini uliokuwa ukisafirishwa kwenda nje ya nchi, huku akiwataka wanasheria kuungana pamoja kwaajili ya maslahi mapana ya Tanzania.
“Kwa kampuni hii inayojiita Acacia, muwaite kwanza muwadai hela zetu, kabla hata ya kusajili, wakubali kwamba tuliwaibia na tubatubu na tunalipa, tuko tayari kukaa kwa makubaliano, ninasema kwa sasa hakuna mchanga utakaotoka kwenda nje,” amesema rais Magifuli.
Aidha, Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kuunda timu ya wanasheria waaminifu ambao watapitia na kuzifanyia marekebisho sheria zote zinazohusu mikataba ya madini ili zipelekwe bungeni kwaajili ya kujadiliwa na kufanyiwa marekebisho.
Amesema kuwa sheria hizo zinapaswa zipelekwe bungeni hata kama ni kwa bunge kuongezewa muda ili ziweze kujadili nakufanyiwa marekebisho kwa maslahi mapana ya Taifa. Aidha ameelezwa kushangazwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kushindwa kuwa na rekodi ya usafirishwaji wa dhahabu pamoja na Wizara ya Nishati na Madini kufanya kazi na kampuni ya Acacia bila kujua kama haijasajiliwa.
“Ukiwa na mali yako kwa mfano umepeleka pamba Ulaya, unapata rekodi kwamba safari hii tumepeleka tani kadhaa, je dhahabu, tunaona ni ya hovyo tu…Wizara yaNishati haikujua kama inafanya kazi na mtu ambayo hajasajiliwa, unafanya nae kazi toka mwaka 1997, unawatuma TMAA wakamkague, hata siku moja hujawahi kumwambia wewe cheti chako kiko wapi,” amesema.

Waziri Mpango ataja vipaumbele vya Serikali katika bajeti ya 2017/18



Serikali imeainisha maeneo ya kipaumbele kwa mwaka 2017/2018 kulingana na mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka ujao wa fedha.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema hayo leo Bungeni mjini Dodoma alipokuwa akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018.

Dkt. Mpango amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na miradi ya kielelezo ya maendeleo ambayo inayolenga kufanikisha utekelezaji wa Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ni pamoja na miradi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma, Mchuchuma Liganga, ujenzi wa reli ya kati kutoka Dar es salaam, Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa km 1,251 kwa “Standard Gauge” pamoja na matawi yake ya Tabora kupitia Isaka hadi Mwanza yenye urefu wa km 379, Isaka hadi Rusumo km 371, Kaliua kupitia Mapanda hadi Karema km 321, Keza hadi Ruvubu km 36 na Uvinza hadi Kelelema kuelekea Musongati yenye urefu wa km 203.

Miradi mingine ya kielelezo ni uboreshaji wa Shirika la Ndege TAanzania (ATC), ujenzi wa mitambo ya kusindika gesi mkoani Lindi, uanzishwaji wa Kanda Maalum za Kiuchumimkoani Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Ruvuma, uanzishwaji wa kituo cha biashara cha Kurasini, kusomesha vijana katika stadi za mafuta na gesi, uhandisi na huduma za afya.

Waziri Dkt. Mpango ameyataja maeneo mengine ya kipaumbele kuwa ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa kukuza uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo y uchumi na maendeleo ya watu, mazingira ya wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji, ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi pamoja na maeneo mengine muhimu kwa ukuaji wa uchumi na ustawi wa taifa.
Dkt. Mpango amesema kuwa shabaha ya uandaaji wa mpango wa bajeti ya mwaka 2017/18 unaongozwa Serikali kusimamia mambo ya uchumi kwa ujumla ikiwemo kuongeza kasi ya ukuaji wa pato halisi la taifa kufikia asilimia 7.5 kwa mwaka 2017, asilimia 7.9 mwaka 2018 na asilimia 8.2 mwaka 2019, kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja kufikia asilimia 5.0 katika kipindi cha muda wakati, kuwa na pato ghafi la taifa la sh. trilioni 123.9 kwa mwaka 2017/18, sh. trilioni 139.7 kwa mwaka 2018/19 na sh. trilioni 165.4 mwaka 2019/20 pamoja na mapato ya kodi kufikia asilimia 14.6 ya pato la taifa mwaka 2017/18, asilimia 15.5 mwaka 2018/19 na asilimia 15.8 mwaka 2019/20.

Aidha, ametaja misingi ya mpango na bajeti kuwa ni amani, usalama, utulivu na utangamano wa ndani ya nchi na nchi jirani ambavyo vitaendelea kudumishwa nchini.
Kuhusu mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018, Dkt. Mpango amesema amewaagiza Maafisa Masuuli kuzingatia masuala muhimu wakati wa uandaaji wa mipango na bajeti za mafungu yao ili kutekeleza Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015.
Zaidi ya hayo, Dkt. Mpango amesisitiza uwepo usimamizi na udhibiti wa matumizi, ulipaji na ongezeko la madeni ya Serikali, ukusanyaji wa mapato pamoja na mfumo wa utoaji taarifa za utekelezaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti Hawa Ghasia alipokuwa akitoa taarifa ya kamati yake amesema kuwa Kamati yake inardhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kusimamia Sheria ya Bajeti na kanuni zake ambayo inahakikisha usimamizi na uwajibikaji katika hatua zote za mchakato wa bajeti unazingatiwa.

Naye Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Halima Mdee alipokuwa akiwasilisha hotuba yake amesema kuwa Kambi Rasmi inaunga mkono hatua za kisheria zinazochukuliwa na Serikali kwa wale wote waliohusika kwa namna moja au nyingine kuhujumu uchumi wa nchi.
Mkutano wa Tano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uanatarajiwa kuhitimishwa Novemba 11 mwaka huu huku shughuli mbalimbali za kuishauri Serikali zikiwasilishwa kupitia mijadala ya Wabunge.






Kategori

Kategori