FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

Chuo chatuma mabilioni kwa mwanafunzi kimakosa



DUNIA haikosi vituko na safari hii kituko cha aina yake kimetokea katika sekta ya elimu. Chuo Kikuu kimoja nchini Afrika Kusini kimesema kwamba kilituma kimakosa jumla ya randi milioni 14 ambazo ni sawa na dola milioni moja za Marekani au Sh bilioni 200 za Tanzania katika akaunti ya benki ya mwanafunzi mmoja nchini humo.
Pesa hizo zilitoka kwenye mfuko wa Shirika la kufadhili wanafunzi kimasomo nchini humo la NSFAS. Chuo Kikuu hicho cha Walter Sisulu, kinasema kuwa pesa hizo ziliwekwa miezi mitano iliyopita, huku makosa hayo yakijulikana baada ya risiti ya akaunti ya mwanafunzi huyo kuonesha kuwa na mamilioni ya pesa baada ya kuwekwa katika mtandao wa kijamii.
Chuo hicho kikuu sasa kinachunguza ni kwa nini mwanafunzi huyo hakupiga ripoti ya kuwepo kiasi kikubwa hivyo cha pesa kwenye akaunti yake. Mwanafunzi huyo amekanusha madai hayo.
Ripoti ya Shirika la Habari la EWN inasema picha zimeonekana kwenye mitandao ya kijamii, zikionesha mwanafunzi huyo wa kike akijisifu na kujionesha kwenye sherehe moja huku akijiburudisha na vitu vizuri vizuri, kama vile simu mpya ya mamilioni ya shilingi.
Inaaminika kwamba mwanafunzi huyo tayari ametumia randi 400,000. Msemaji wa Chuo hicho Kikuu Yonela Tukwayo, amesema kuwa pesa hizo ziliwekwa kwenye akaunti hiyo kimakosa na kampuni ambayo inasimamia fedha za hazina ya kitaifa za msaada wa karo ya wanafunzi (NSFAS) ambayo inajulikana kama Intellicard na kwamba ni sharti mwanafunzi huyo arejeshe fedha hizo: “Pia tunaangalia sheria za NSFAS, inayoonesha mtoto huyo alitia saini makubaliano ya kukubali.... Masharti ya matumizi ambayo fedha hizo zinafaa kutumika.
“Kwa hivyo itabidi mwanafunzi huyo alipe kila senti ya fedha alizotumia, hata akilipa kwa miaka 20 na zaidi.” Maofisa wa NSFAS wamekanusha madai hayo, wakisema kuwa chuo kikuu hicho cha Walter Sisulu ndicho kinachofaa kulaumiwa.
Gazeti moja nchini Afrika Kusini limewauliza wasomaji ni kwa njia gani wangetumia pesa nyingi kama hizo iwapo wangeamka na kuzipata kwenye akaunti. Shirika la Habari la News24 baadaye limemnukuu msemaji wa chuo kikuu hicho Yonela Tukwayo, akisema kuwa kuhamishwa kwa fedha hizo hadi kwenye akaunti isiyokusudiwa, yalikuwa ni makosa ambayo yangegunduliwa na NSFAS, ambayo inasimamia malipo hayo.
NSFAS imekanusha madai hayo kupitia msururu wa ujumbe kwenye Twitter, huku ikisema kuwa si yenye kulaumiwa kwa makosa hayo. Tukwayo anasema kuwa, mwanafunzi huyo tayari ametumia, dola 38,000 (£30,000), huku akitakiwa kulipa kila ‘’senti aliyotumia’’.
Ripoti hiyo inasema kuwa mwanafunzi huyo anashikilia wadhifa wa uongozi katika chama cha wanafunzi wa Chuo Kikuu. Mwenzake katika chama hicho cha wanafunzi wa Chuo Kikuu, ameiambia News24 kuwa, ujumbe katika mtandao wake wa kijamii wa Facebook unadai kuwa amepokea fedha hizo kwa njia halali.
Ujumbe wa mwanafunzi huyo unasema kuwa pesa hizo tayari zimerejeshwa: “Jibu ni rahisi, NSFAS ilifanya makosa kwa kuweka pesa nyingi katika akaunti isiyokusudiwa na akaunti hiyo ikawa ni yangu. “Kwa hivyo sikanushi chochote, pesa kwa hakika ziliwekwa tarehe 1 mwezi Juni na kurejeshwa Agosti 13.”