FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

UHURU KENYATTA AONGOZA KATIKA UCHAGUZI WA RAIS KENYA, UPINZANI WAPINGA MATOKEO


Kinara wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amepinga matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais uliofanyika jana Jumanne, yanayoonyesha kuwa Rais wa sasa Uhuru Kenyatta anaongoza.
Akihutubia waandishi wa habari jijini Nairobi jana usiku, Odinga ambaye amewania kiti hicho kupitia ODM, chama tanzu katika muungano wa upinzani wa NASA ameyataja matokeo hayo kama ‘bandia’ na yasiyoakisi uhalisia wa mambo na matakwa ya Wakenya.
Waziri mkuu huyo wa zamani amesema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC inastahili kuwapa mawakala wa vyama Fomu Nambari 34A kutoka vituoni kabla ya matokeo kutangazwa na kwamba kinachofanyika sasa ni sawa na ‘tarakilishi kupiga kura’.
Awali wakala mkuu wa muungano huo wa upinzani, Musalia Mudavadi alihutubia wanahabari na kutaja matokeo yanayotangazwa na tume hiyo katika tovuti yake kama utapeli, huku akitoa wito kwa wafuasi wa mrengo huo kupuuzilia mbali matokeo hayo.
Hadi tunaenda mitamboni, kwa mujibu wa tovuti ya matokeo ya IEBC, Rais Uhuru Kenyatta ambaye anawania muhula wa pili kwa tiketi ya Chama cha Jubilee anaongoza kwa kura miliioni 6.9, sawa na asilimia 53 , huku Odinga akimfuata kwa karibu kwa kura milioni 5.4, sawa na asilimia 45 ya kura milioni 12.5 zilizohesabiwa kufikia sasa.
Ili kuibuka mshindi na kuepusha kuingia duru ya pili ya uchaguzi, mshindi wa uchaguzi wa urais nchini humo anahitaji kupata asilimia 50+1 ya kura, na kwa akali asilimia 25 kutoka kaunti 24, kati ya kaunti 47 za nchi hiyo.