FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

‘Nyama ikae saa nane kabla ya kupikwa’




NYAMA nyekundu ni kitoweo kitokanacho na wanyama. Mbali na wanyama wa porini, watu wengi hupata nyama hiyo kutokana na kuchinja wanyama wafugawao kama ng’ombe, mbuzi, kondoo na ngamia.
Nyama nyekundu hutakiwa kuandaliwa kwa umakini iwe salama na bora kwa afya ya mlaji tofauti sana na inavyoandaliwa mara nyingi na Watanzania wengi. Ofisa Mifugo Bodi ya Nyama Tanzania, Ezekiel Maro, anasema nyama bora na salama inayotakiwa kuliwa ni iliyochinjwa na kuwekwa katika chumba chenye baridi (chilling) kuanzia saa nane hadi 24 kuruhusu misuli kufa na kutengeneza nyama.
Anasema nyama inayoliwa na wengi huwa ni msuli kutokana na kutokaa saa nane hadi 24 kabla ya kuliwa. Akizungumza kwenye maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa (DITF), Maro anasema zipo athari za nyama inayoliwa kabla ya kukaa muda huo. Athari hizo anasema ni pamoja na kuwa na kiasi kikubwa cha tindikali, kukosa ulaini pamoja na ladha.
Akizungumzia kuhusu hali ya ulaji wa nyama nchini, mtalaamu huyo anasema mtanzania anakula wastani wa kilo 15 za nyama kwa mwaka wakati kiwango halisi kinachotakiwa ni kilo 50 kwa mwaka.
Hivyo anasema wananchi wanapaswa kufahamu kuhusu ulaji wa nyama bora na salama, waelewe kuhusu biashara ya nyama namna inavyofanyika na pia waelewe majukumu ya Bodi ya Nyama.
Vilevile anasema wananchi wanatakiwa kuelewa kwa kina kuhusu suala la kufungulia wawekezaji fursa zote zinazopatikana katika mnyororo wa thamani wa nyama nchini na pia wadau waweze kufahamu matakwa yao ya kisheria katika kuzalisha uzalishaji ulio bora.
Kuhusu biashara ya mifugo, Maro anasema inatakiwa iwe inafanyika katika minada ambayo idadi yake kwa sasa nchini kote ni takribani 550 ikiwemo inayofanya kazi kila siku na ile ambayo ni ya mzunguko.
Katika minada, anasema wafugaji wanatakiwa kupeleka mifugo yao na kuwe na sehemu ya kunadia, ambapo kwa sasa katika minada muuzaji na mnunuzi hupatana kuhusu mifugo yao, yaani huweza kunong’ona kabla ya mnada kufanyika.
Minada inatakiwa kusajiliwa na Bodi ya Nyama, huku ikitakiwa kuwa na kiringe, mpiga sauti sambamba na kuwepo kwa miundombinu thabiti ili kuiwezesha bodi kufikiria namna ya kupanga bei ya nyama.
Maro anasema bodi inafikiria namna ya kuanza kupanga bei elekezi ya nyama kuanzia mwakani na kwamba kwa sasa wanakamilisha uwepo wa miundombinu sahihi ya kupimia mifugo katika kila halmashauri.
Katika kupanga bei anasema ni lazima kuwe na kanuni ambayo haitomuonea yeyote. Itakuwa ni kanuni yenye usawa na haki ingawaje bei hiyo haiwezi kufanana maeneo yote nchini.
Aidha anasema bodi hiyo haiwezi kuanza kupanga bei hiyo mpaka kuwe na miundombinu sahihi ya kupima mifugo ambapo kwa sasa wanaelekeza halmashauri kufunga mizani ya kidijiti katika minada.
Katika maeneo ya minada anasema ni lazima kuwe na kiringe na pindi wakimaliza wataweza kuanza kupanga bei. Katika kuhakikisha hatua hiyo inafikiwa, Maro anasema Bodi itaimarisha vyama vya wadau wa nyama kama vyqma vya wafugaji,wafanyabiasharawa nyama na mifugo, wasindikaji na hata vyama vya mifugo ya nguruwe.
Tayari Bodi imewajengea uwezo wanachama hao ili kuwa imara na kuweza kusimamia sekta ya nyama kwa umakini. Bei elekezi ya nyama itapangwa kwa kuangalia uzito halisi wa mnyama kabla ya kuchinjwa na endapo atakuwepo mdau atakayeuza kwa bei nyingine wahusika katika vyama hivyo wataingilia kati.
Anasema kwa Bodi kupanga bei ya nyama walaji wategemee kupata thamani ya fedha yao kwa ubora wa nyama huku biashara ya nyama ikitakiwa ifanywe katika nyumba maalumu zilizoidhinishwa na kwamba itakuwa ni marufuku kwa machinjio kuuza nyama.
Kuhusu biashara ya nyama, Digna Mallya, Ofisa Mifugo katika bodi hiyo anasema mabucha yameopangwa na bodi kwa madaraja kuanzia la kwanza, pili na hata daraja la juu.
Anasema kwa bahati mbaya wauzaji wengi kwenye mabucha hawajui namna ya kuuza nyama kwa kuzingatia usafi kutokana na kuacha nyama iking’ong’wa na nzi. Bodi inafikira kutengeneza kanuni ili wauzaji wawe na vyeti, na kuhakikisha wanaheshimika na walaji kuliko ilivyo sasa.