FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

Dk Mwakyembe: Chagueni viongozi wasafi TFF


LEO unafanyika Uchaguzi Mkuu wa TFF ambapo macho yote ya Watanzania yapo Dodoma kufuatilia uchaguzi huo ambapo atapatikana Rais wa kuliongoza Shirikisho hilo lenye dhamana ya kukuza mpira wa miguu nchini.
Katika hotuba yake kwa wajumbe waliohudhuria mkutano huo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harison Mwakyembe amewaambia wajumbe kuwa wanatekeleza jukumu jukumu muhimu la Kikatiba ya nchi.
Amewakumbusha wajumbe kuwa watanzania wana matumaini makubwa na wanawaamini katika kuwachagulia viongozi bora watakaoendeleza mpira wa Tanzania na hatimaye kulipaisha taifa katika ulimwengu wa kandanda.
“Viongozi bora huibuliwa na wajumbe makini wasioyumbishwa na vishawishi vya rushwa wanao ongozwa na dhamira njema na uzalendo,” amesema Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harison Mwakyembe katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano.
Ameongeza kuwa Mafanikio ya Michezo hayaji bila kujenga mazingira bora yakufanikiwa hivyo wajumbe wamebeba dhamana kubwa ya Michezo, na wanatakiwa kuwatendea haki Watanzania kwa kuwachagulia viongozi waadilifu.
Kwa mara ya kwanza viongozi wa TFF wataapishwa mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu. Kinachotakiwa kwa wajumbe wa mkutano ni kuonesha ukomavu wa Kidemokrasia ili soka la Tanzania lipate mkombozi.
“Tunataka uongozi utakao isimamia Serengeti Boys ili iweze kushiriki mashindano ya Olympic ya vijana.Tunataka uongozi utakao shirikiana na Serikali kuwaendeleza vijana waliopatikana kutoka katika Michezo ya UMISETA,” amesema Waziri Dk Mwakyembe.
“Tunataka viongozi wanaofahamu kuwa FIFA na CAF hawakumbatii rushwa. Tunataka viongozi wanaofahamu kuwa Serikali ya awamu ya tano inapiga vita rushwa na ubadhirifu,” Ameongeza.
Katika hotuba hiyo, Waziri Mwakyembe ameweka wazi kuwa kama kuna mtu anatafuta uongozi ili kujipatia fedha huyo amepotea njia. Amesema Serikali itaendelea kuboresha Michezo na miundombinu ya michezo nchini.
Pia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuheshimu Uhuru wa vyama vya Michezo nchini ila haitovumilia ubadhirifu na rushwa na ufisadi kwa sababu unahujumu uchumi wa Taifa. Imeandaliwa na Idara ya Habari-MAELEZO