VIONGOZI wa dini nchini wametakiwa kutumia nafasi zao kuelimisha umma kuhusu matumizi sahihi ya huduma ya mitandao ya kijamii ili kujiletea maendeleo.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa wakati wa futari
iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na
Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema ni vema viongozi wakatumia
nafasi zao kueleza matumizi sahihi na huduma za mitandao ya kijamii katika
kueneza imani na kujiletea maendeleo binafsi na taifa kwa jumla.
Waziri Mbarawa alitoa mfano wa
machafuko ya nchi ya Misri ya mwaka 2011 yaliyodumu hadi sasa kuwa yametokana
na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kutokana na ujumbe wa mtu mmoja
aliouandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa
wa Dar es Salaam, Shehe Alhad Mussa Salum alisema Kamati yao imefanya mambo
mengi kuhakikisha kunakuwapo amani na utulivu nchini.
Shehe Salum alitumia fursa hiyo
kuwataka Waislamu kutumia kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu Ramadhan kuleta
amani miongoni mwa watu wa imani na dini mbalimbali. Mkurugenzi Mkuu wa TCRA,
James Kilaba alisema ukuaji wa teknolojia umekuja na changamoto nyingi
zinazohitaji ushirikiano na wadau mbalimbali kuzishughulikia.