UTALII ni miongoni mwa shughuli zinazogusa asilimia kubwa ya maisha ya wanadamu. Inasadikiwa neno utalii au ‘Tourism’ kwa lugha ya Kiingereza lilianza kutumika duniani miaka ya 1700.
Ingawa zipo takwimu zinazoonyesha tangu kuumbwa kwa dunia utalii ulikuwepo ingawa haukuwa rasmi. Wanatajwa wasafiri kama vile Marco Polo kartika karne ya 13 pamoja na safari za kina Dk David Livingstone waliogundua mambo mengi kuanzia bara la Asia hadi Afrika, taarifa zao zinaeleza mengi juu ya utalii walioufanya. Hata hivyo kabla ya miaka ya 1950, utalii ulikuwa ni ule wa mtu kutoka nchi moja kwenda nyingine kwa elimu au matembezi.
Utalii haukuchukuliwa kama shughuli rasmi inayoweza kutazamwa kuwa sehemu ya kuinua taifa kiuchumi. Wanahistoria wanasema miongoni mwa sababu zilizokuza utalii duniani ni wanadamu kuongeza kipato, kuwa na muda wa ziada na haja ya kujifunzia mazingira ya ulimwengu na vivutio vyake pamoja na sababu za kidini. Ndio maana kuna utalii wa kitamaduni, kijamii, kidini, kimatibabu na kibiashara. Aina zote za utalii zinafanya kazi na ni sehemu kubwa ya mapato kwa mataifa husika.
Njia pekee ya kuvutia watu kutembelea maeneo mazuri taifa iliyonayo ni kujitangaza. Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania, Profesa Jumanne Maghembe wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara hiyo bungeni hivi karibuni alisema mwaka 2016 Tanzania ilipokea watalii zaidi ya milioni 1.2 ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.9 ikilinganishwa na mwaka 2015 walipokuja watalii mil 1.1.
Kutokana na idadi hiyo ya watalii mwaka jana sekta ya utalii iliingiza Dola za Kimarekani bilioni mbili ikiwa ni sawa na sh trilioni nne mwaka 2015 iliingiza dola bilioni 1.9. Kiwango hicho cha mapato kiliifanya sekta ya utalii kuchangia asilimia 17.5 ya pato la taifa katika bajeti ya mwaka 2016/17 pamoja na kuingiza asilimia 25 ya fedha za kigeni. Taarifa za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Utalii Duniani ( UNWTO), zimeitaja China kuwa taifa namba moja kwa soko la utalii ulimwenguni.
Mwenyekiti wa TTB, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo alipata kusema, “Bado nchi yetu inajipambanua kwa amani duniani, wageni wengi wanavutiwa kuja kufanya shughuli mbalimbali za kisanii na kujifunza utamaduni wetu kutokana na sifa kubwa ya amani na utulivu, tuzilinde tunu hizi ili waje wengi zaidi.” Huu ni ujumbe kwa wananchi walio katika maeneo ya kitalii. Ukarimu wetu na namna nzuri ya kuwapokea wageni ndiyo silaha pekee ya kuvuta watalii wengi zaidi.
Msingi wa maelezo hayo ni ziara ya siku tatu nchini Israeli iliyofanywa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Devota Mdachi aliyeongozana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dk Aloyce Nzuki. Katika ziara hiyo iliyofanyika hivi karibuni, pamoja na mambo mengine ilikuwa na lengo la kukutana na wadau wa sekta ya utalii wakiwemo mawakala wa utalii na sekta ya malazi.
Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam baada ya kurejea katika ziara hiyo, Mdachi anasema: “Israeli imeonyesha shauku kubwa ya kushirikiana na sisi katika kuutangaza utalii wa Tanzania.” Anasema mwaka, Tanzania ilipata watalii 22,000 kutoka nchini humo na kwamba wameahidi mwaka huu watakuja watalii wengi zaidi. “Shlomo Carmel, mmiliki wa kampuni ya Another World, ameahidi kuleta watalii zaidi ya 2000 kati ya Agosti na Desemba mwaka huu.”
Hii ni habari njema kwa Watanzania na sekta ya utalii. Fursa kama hii zinapojitokeza, huonekana ni za watu maalumu. Lakini kimsingi, ni fursa za Watanzania wote bila kujali shughuli zinazofanyika. Takwimu zinaonesha mwaka 2011 watalii waliingiza dola za Kimarekani trilioni 1.03 ulimwenguni. Hii ni sawa na Sh trilioni 2,000. Unaweza kujiuliza fedha hizi zinaingiaje?
Watalii ni wanadamu na mara nyingi wanapofanya shughuli zao za kitalii wanajipanga kwa miaka kadhaa kuweka fedha. Hivyo kila wanachofanya, wanahitaji kutoa fedha ambazo wapokeaji ni wananchi wa eneo alilofanya utalii. Kuna suala la malazi kwa maana ya hoteli, chakula, mavazi, huduma kama kuelekeza au kubeba mizigo pamoja na malipo yanayohusu vibali vya kuingia nchi husika.
Balozi wa Tanzania nchini Israeli, Jacob Massima alikuwa sehemu ya ziara ya watendaji hao wa TTB. Anasema ingawa amekaa muda mfupi na Waisraeli, lakini ameona namna wanavyopenda kusafiri, na hii ni fursa muhimu kwa sekta ya utalii nchini. “Nimeona namna Waisraeli wanavyotumia muda mwingi kusafiri na hasa wanavyoipenda Tanzania, nami nimeona namna vivutio vilivyopo hapa vinavyofaa kwa Watanzania kuja kutalii.
“Tunasema hii ni nchi takatifu, waumini wa dini zote duniani wanaguswa na namna moja au nyingine kuja kutembelea. Hivyo nitatumia nafasi yangu ya ubalozi kuwa kiunganishi kwa Tanzania na Israeli kwenye sekta hii muhimu ya utalii,” anasema Balozi Massima. Kwa sasa dunia inaitumbulia macho China, nchi ambayo ina wakazi zaidi ya bilioni 1.4, ambao asilimia kubwa wanapenda kutalii na kujifunza maisha mapya.
Takwimu zinaonesha Wachina milioni 300 wamefanya ziara ndani ya taifa lao. Hii inaonyesha ni namna gani wanapenda kusafiri. Hivyo ikiwa watu hawa watashawishiwa kujua miji mipya kwa kujitangaza maana yake ni soko zuri kwa mataifa yenye vivutio vingi vya utalii ikiwemo Tanzania.
Hata hivyo, kumekuwapo na hali inayoonesha kuwa tumeshindwa kutumia vizuri fursa hii kwa sababu takwimu zinaonesha mwaka jana watalii 30,000 pekee ndio wameingia nchini kutoka China.
Hii ni idadi ndogo ambayo inapaswa kifanyike kitu cha maana kuiongeza. Si kwa China na Israeli tu, bali Tanzania ina mataifa mengi ya kuyavutia kwenye utalii. Hata ndani ya nchi, bado upo mwamko mdogo wa kuzungukia mbuga za wanyama na maeneo mengine ya vivutio.
Vipo vivutio vikitajwa dunia nzima itatamani kufika katika ardhi hii na kukaa hata mwaka mzima wasivimalize. Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zenye mbuga ya wanyama pembezoni mwa bahari. Mbuga hii ni hifadhi ya Saadan.
Ngorongoro crater ni miongoni mwa maajabu ya dunia. Kilimanjaro ambao ni mlima mrefu kuliko yote Afrika upo Tanzania. Visiwa vyenye fukwe safi, mbuga zenye wanyama wengi na ule msimu mahsusi wa nyumbu kuhama kutoka taifa moja kwenda jingine, yote haya yanapatikana Tanzania.
Kama hiyo haitoshi, Ziwa Tanganyika lina sifa nne za kidunia. Kwanza ndilo ziwa refu kuliko yote duniani, ndilo ziwa la pili lenye kina kirefu duniani, ndilo ziwa la pili lililojulikana miaka mingi kuliko yoye duniani na ndilo ziwa la pili kuwa na maji mengi duniani.
Vivutio hivi ni neema kwa Tanzania ambavyo hata hivyo, nchi inahitaji kujitangaza zaidi kwa lengo la kuvuta watalii waliingizie taifa pato. Huu ndiyo wajibu wa Bodi ya Utalii Tanzania.