MSHAMBULIAJI wa Yanga, Simon Msuva, amesononeshwa na kitendo cha uongozi wa timu hiyo kuamua kuachana na mshambuliaji mwenzake Haruna Niyonzima.
Akizungumza na gazeti hili katika kambi ya timu ya Taifa, Msuva alisema kukosekana kwa Niyonzima kwenye kikosi hicho ni pigo kwake, kwani walikuwa wakicheza kama pacha. “Wote tunacheza upande wa kushoto lakini pia Niyonzima alikuwa anacheza kulia na mara nyingine tulikuwa tunabadilishana, hivyo kukosekana kwake kunanitia simanzi sana,” alisema Msuva.
Kauli ya Msuva imekuja juzi baada ya uongozi wa Yanga kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Boniface Mkwassa kutangaza kuachana na Niyonzima baada ya kushindwa kufikiana dau la usajili kwani mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwezi ujao.
Yanga walimtaka Niyonzima kwa miaka miwili mingine lakini walishindwana baada ya kutaka kulipwa dola za Marekani 60,000 karibu ya sh milioni 120 za Kitanzania na inasemekana amesajiliwa na mahasimu wao Simba.
Niyonzima alijiunga na Yanga misimu sita iliyopita akitokea APR ya Rwanda na ameisaidia kupata mataji sita, manne ya Ligi Kuu, moja la Kombe la Kagame na lile la FA.