POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imewaonya watu waliojipanga kufanya uhalifu katika sikukuu ya Eid El Fitr.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Lucas Mkondya alisema, kuelekea sikukuu hiyo ulinzi umeimarishwa vilivyo ili kuhakikisha wananchi wanasherehekea kwa usalama.
“Jeshi la polisi limejipanga vizuri katika kufanya doria za masaa 24 katika maeneo yote ya jiji hasa maeneo yenye viashiria vya uhalifu, pia patakuwa na doria na doria maeneo ya misikitini, kumbi za starehe na mikusanyiko mikubwa ya watu,” alisema Kamanda Mkondya.