FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

Uchaguzi waahirishwa ngome za upinzani magharibi mwa Kenya


Polisi wakikabili mwandamanaji Katwekera, Kibera


Tume ya Uchaguzi nchini Kenya imetangaza kuahirishwa kwa uchaguzi wa marudio katika majimbo manne magharibi mwa nchi hiyo ambayo ni ngome ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliyetoa wito kwa wafuasi wake kususia uchaguzi wa leo.
Watu wawili wameuawa kwa kupigwa risasi wakati wa makabiliano kati ya polisi na wafuasi wa upinzani katika maeneo hayo.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amesema tume imechukua hatua hiyo baada ya upigaji kura kutatizwa na ukosefu wa usalama.
Katika majimbo hayo ya Kisumu, Siaya, Migori na Homa Bay, wafuasi wa upinzani walifunga barabara za kuelekea katika vituo vya kupigia kura na kukabiliana na maafisa wa polisi siku yote.
Katika baadhi ya maeneo, makarani na maafisa wengine wa kupigia kura hawakufika vituoni kutokana na kile mmoja wa wasimamizi alisema ni kuhofia usalama wao.
Serikali ilikuwa imewatuma maafisa wa polisi katika maeneo mbalimbali kushika doria.
Gavana wa jimbo la Kisumu Prof Anyang' Nyongo amewatuhumu polisi kwa kutumia "magenge ya watu" kuwashambulia wafuasi wa upinzani.
Ameambia BBC kwamba watu wawili wamefariki eneo lake na wengine 29 wanauguza majeraha.
Prof Nyong'o amesema hawataruhusu uchaguzi wa marudio ufanyike katika kaunti hiyo.
"Nimetangaza kama gavana wa hii kaunti wiki moja ya maombolezi ambapo wakati huo hakutakuwa na sherehe. Kwetu uchaguzi huwa ni sherehe," amesema.
Amesema iwapo tume hiyo itaendelea kusisitiza uchaguzi ufanyike, basi wataenda kortini kutaka uzuiwe.

Wapiga kura wachache kujitokeza

Ni wapiga kura wachache waliojitokeza kupiga kura leo ikilinganishwa na uchaguzi wa kwanza uliofanyika tarehe 8 Agosti.
Rais Kenyatta, ambaye anatarajia kuibuka mshindi, alikuwa amewahimiza wapiga kura kujitokeza kwa wingi.

Mpinzani wake mkuu Bw Odinga hata hivyo alikuwa amesema uchaguzi huo si wa kuaminika na kuwataka wafuasi wake kutoshiriki.
Uchaguzi wa leo ulitokana na hatua ya Mahakama ya Juu ya kufuta matokeo ya uchaguzi huo wa Agosti kutokana na kesi iliyowasilishwa na Bw Odinga.
Mahakama hiyo ilisema uchaguzi huo ulijaa kasoro nyingi ambazo kuna uwezekano ziliathiri matokeo.

Usalama kudumishwa

Maelfu ya maafisa wa polisi, wakisaidiwa na maafisa kutoka idara nyingine za usalama, walikuwa wametumwa kudumisha usalama katika vituo vya kupigia kura kote nchini humo pamoja na kutoa ulinzi wa wapiga kura.
Vituo vya kupigia kura vilifungwa saa kumi na moja jioni, ingawa katika baadhi ya maeneo ambayo vituo vilichelewa kufunguliwa muda wa kufunga vituo uliongezwa.
Bw Chebukati alisema ingawa upigaji kura uliendelea vyema katika baadhi ya maeneo, kuna maeneo yaliyoathiriwa na hali ya usalama pamoja na mvua kubwa iliyonyesha maeneo mengi na kutatiza usafiri.

Kaunti nne ambazo uchaguzi umeahirishwa 
 Makundi mengi ya waangalizi wa kimataifa yalikwua yamepunguza idadi ya waangalizi kutokana na wasiwasi wa kiusalama.
Matokeo ya kutoka vituo vya kupigia kura, yaliyo kwenye fomu zifahamikazo kama Fomu 34A, yamekuwa yakipakiwa katika mtandao wa tume hiyo.
Matokeo ya jumla ya matokeo ngazi ya maeneo bunge ambayo hutolewa kupitia Fomu 34B yanatarajiwa kutolewa baadaye.
Tume ina hadi siku saba kutangaza matokeo ya jumla ya urais, ambayo hutangazwa kupitia Fomu 34C.



Uhuru Kenyatta na mpiga kura - 26 October 2017
Rais uhuru kenyata akitoka kupiga kura

Kuchoshwa na siasa

Baada ya kupiga kura Gatundu, Bw Kenyatta alisema wakati umefika kwa taifa kusonga mbele.
"Tumechoshwa na kuwa katika kipindi cha uchaguzi. Ni wakati wa kusonga mbele," alisema.
 Aliongeza pia kwamba maeneo mengi nchini humo usalama ulidumishwa.