FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

MAKOSA 8 YANAYOFANYWA NA WATU WA KIPATO CHA KATI KWENYE MATUMIZI YA FEDHA


Kundi la watu wenye kipato cha kati linahusisha walimu, askari, wakandarasi, mameneja wa ujenzi nk. — kwa kifupi ni wafanyakazi wote wenye mchango mkubwa katika kujenga uchumi wa Taifa. Kundi hili hutoa na kutumia huduma mbalimbali na kuifanya jamii iendelee, kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi kwa kodi inayokusanywa kutoka katika kila bidhaa au huduma wanayonunua.
Lakini linapokuja suala la fedha, tabaka la daraja la kati linakumbana na changamoto za kipekee za aina yake. Ongezeko dogo la kipato, kushuka kwa thamani ya pesa, kupanda kwa gharama za kodi za nyumba na huduma za afya kunazidi kufanya kipato kisitosheleze mahitaji. Kwa hali kama hii, watu wengi wa daraja hili hawana uwezo wa kujiwekea akiba ya kuwawezesha kuwa na maisha salama uzeeni baada ya kustaafu.
Lakini je, matatizo yote tunayoyapata kwenye maswala ya fedha yanatokana na uchumi? Hapana! Kama ilivyo kwa watu kwenye makundi mengine ya kipato, wengi wetu hatufanyi maamuzi sahihi yatakayotusaidia linapokuja jambo la matumizi ya pesa tunazopata. Kama watu wa daraja la kati wanatarajia kuwa na maisha mazuri baadae, ni juu yetu kufanya maamuzi sahihi bila kujali nini kinatokea kwenye uchumi wa nchi kwakuwa hatuwezi kuzuia uchumi wa nchi usiimarike au kuporomoka – lakini tunaweza kuamua tutumie vipi pesa iliyopo mfukoni. Yafuatayo ni makosa nane yanayofanywa na watu wa kipato cha kati ambayo wanaweza kuyaepuka na kubadili hali zao kabisa:
1. Madeni mengi
Tafiti zinaonesha kuwa watu wengi wa kipato cha kati wana madeni – wengine ni kutokana na sababu za msingi lakini wengi wao ni kwa sababu za kufanya matumizi ambayo yangeweza kuepukwa.
Kwa watu wa tabaka la kipato cha kati wanaotarajia kupata mafanikio ya kifedha, tabia hii ya kujiingiza kwenye madeni kirahisi ni kosa kubwa sana litakalosababisha majuto uzeeni au mara baada ya kustaafu.
Wataalamu wa maswala ya fedha wanasema kwamba moja ya njia za uhakika za kukufanya uwe na akiba ni kuweka mkakati utakaokusaidia kulipa madeni yako yote kutokana na kipato unachotengeneza kila mwezi. Kwa kufanya hivi utakuwa unabaki na fedha bila kuwa na wasiwasi juu ya madeni uliyonayo, jambo litalokuwezesha kutumia pesa yako kwenye vitu vya msingi zaidi kama kujiwekea akiba ya dharura au kuweka kwenye mfuko wako wa pensheni
2. Kutokuwa na akiba ya dharura
Zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wa kawaida wanahaha sana kuomba michango wanapokutwa na dharura inayohitaji kiwango kikubwa cha pesa kuitatua. Kama sherehe za harusi tu hulazimisha familia za wanandoa husika kupitisha bakuli kwa ndugu, jamaa, majirani na marafiki, bila shaka kwenye dharura ambazo huibuka katika siku na muda usiojulikana, michango hii hukusanywa huku kukiwa na presha ya hali ya juu na kusababisha wakati mwingine ndugu au marafiki kugombana. Tabia yetu ya kutokuwa na utamaduni wa kuweka pembeni kiasi cha pesa kitakachosaidia tunapokutwa na dharura ni tatizo kubwa sana.
Kama huna kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya dharura zitakazotokea — ambazo ni lazima zitatokea tu — inakuwa rahisi sana kwako kutumia vibaya pesa au kujikuta unaingia kwenye madeni ambayo yatakusumbua kuyalipa hivyo kukugombanisha na uwapendao waliokusaidia kwa nia njema kukuokoa kwenye shida iliyokukuta.
3. Kutojiwekea akiba yako ya kustaafu wakati unafanya kazi
Hadi kuweza kufikia umri wa kustaafu ukiwa salama inakuhitaji uishi kwa uvumilivu pamoja na kuwekesa sehemu ya kipato unachoingiza kwa muda wa hadi miaka 40. Kama unatarajia uishi vizuri miaka ya uzeeni mwako, ni muhimu kujiongezea kiwango cha mchango unayoweka kwenye mfuko wako wa pensheni kadri unavyozidi kupata pesa. Kama hutafanya hivyo, itakuchukua muda mrefu zaidi kuweza kuwa na kiasi cha pesa kitachokuwezesha kustaafu kwa amani, ndio sababu wazee wengi wanaolazimika kuendelea kufanya kazi za mikataba au kazi ndogondogo hata baada ya kustaafu kwao.
4. Kutegemea pensheni na kiinua mgongo
Umuhimu wa mchango unaotolewa na kampuni yako au Serikali kwenye mfuko wako wa pensheni hauwezi kudharauliwa lakini kuwa na sehemu moja tu ya kuweka michango yako ya pensheni haitoshi. Sio tu kwamba utajikuta umeshaishiwa utakapofikisha umri wa kustaafu, lakini kuna faida utazozikosa kwa kuwekeza sehemu moja.
Njia mojawapo ya kujihakikishia unatimiza lengo lako ni kujua kiasi cha mchango unaotolewa na kampuni yako au Serikali kwenye pensheni yako na wewe kuhakikisha unaweka kiasi kama hicho kwenye pensheni yako kila mwezi, kisha hakikisha una uwekezaji mwingine japo mdogo ambao unaweza kuweka pesa yako ikawa inakuletea faida kidogokidogo kwa sababu itakusaidia kutokuwa na madeni yatakayokurudisha nyuma baada ya kustaafu kwako.
5. Kutokuwa na bima ya afya
Baadhi ya mifuko mizuri wa bima ya afya duniani inaruhusu wanachama kuendelea kuchangia kwenye mifuko yao ya bima ya afya. Ingawa kanuni za kuratibu uendeshwaji wa mifuko hii zinatofautiana, namna inavyofanya kazi si tofauti sana.
Baadhi ya mifuko inaruhusu kutoa michango yako bila kutozwa kodi yoyote na kisha kulipia gharama zako za kiafya za sasa au baadaye. Kama unaweza, ni bora kuweka michango yako kwenye mifuko yenye huduma kama hizi ukijua kwamba swala la afya yako umeliwekea usimamizi mzuri na hutalazimika kutoa fedha hata ikifika uzeeni ambapo hutakuwa na nguvu za kuendelea kufanya kazi tena.
Faida nyingine ya bima za aina hii ni kumuwezesha mwanachama kulipia gharama za huduma zisizolipiwa na bima za kawaida. Huduma za kuwaona madaktari bingwa wa mishipa ya fahamu, meno au macho ni baadhi ya huduma ambazo bima nyingi za afya hazilipii gharama zake.
6. Kuchelewa kujiwekea akiba ya akiba ya kustaafu
Kosa linalofanywa na watu wengi wenye kipato cha kati ni kuchelewa sana kuanza kujiwekea akiba ya uzeeni watakayoihitaji sana baada ya kustaafu kazi wanazofanya na wakati huo wakiwa wanafanya matumizi yasiyo na lazima sana au kuweka pesa kwenye miradi isiyo na faida endelevu.
Wengi wetu tunajikuta tukijishawishi kwamba tutaanza kuweka akiba ya pensheni baada ya kumaliza ujenzi wa nyumba au baada ya kumaliza mkopo wa gari au baada ya mtoto wa mwisho kumaliza chuo kikuu. Ingawa haya yote ni malengo mazuri na yenye maana maishani, maisha yanaendelea na ni rahisi sana kuweka kiasi kidogo kwenye mfuko maalum, la sivyo utakuja kushtuka ukiwa umechelewa sana.
Kama wewe ni mtu wa kipato cha kati, unahitaji muda mrefu kuweza kuwa na kiasi kikubwa cha fedha kwenye mfuko wako wa pensheni. Wataalamu wanashauri kuanza kujiwekea akiba ya pensheni mapema iwezekanavyo maishani mwako ili kuweza kuona faida hasa ya uamuzi wako kwakuwa kiasi kidogo cha fedha unachochangia kila mwezi bila kukosa kitasababisha uwe na pesa zitazokutosha baada ya kustaafu kwako. Unaweza kuanza kuchangia asilimia 1 tu ya kipato chako kila mwezi na kuongeza kidogo kidogo mpaka itakapofika asilimia 10 au 15.
7. Kutoorodhesha warithi wako kwenye taarifa za mfuko wa kustaafu, bima ya maisha na akiba zako
Ni kweli kwamba unataka pesa kutoka kwenye bima yako ya afya zichukuliwe na mtalaka wako? Vipi kuhusu wazazi wako kuchukua pensheni yako? Haya ndio mambo yanayotokea unapojisahau kuboresha taarifa za mabadiliko ya warithi wako ikitokea umefariki dunia.
Ndoa, talaka au mabadiliko yoyote yanayotokea kwenye familia ni sababu tosha za kurudi na kurekebisha taarifa zako. Taarifa hizi za watu wanaostahili kupewa pesa iliyopo kwenye mifuko unayochangia zinalindwa kisheria na zinazidi nguvu hata ya mirathi uliyoandika. Kwahiyo, mtu yeyote aliyetajwa kwenye fomu hizo atapewa pesa hizo bila kujali karatasi zako za mirathi zinasema nini.
Jambo hili linatokea mara nyingi kuliko watu wanavyodhani: Hakuna hata mtu mmoja anaefikiri atakufa akiwa kijana, lakini tunajionea vijana wengi wanakufa kila kukicha na kama taarifa kwenye mifuko unayochangia hazijaboreshwa, kiasi kikubwa cha pesa zako kinaweza kwenda kwenye mikono ambayo hukupanga kwenye uhai wako.
8. Kununua vitu vingi vinavyoshuka thamani
Sababu moja tu kwamba kitu kama gari kinashuka thamani mara moja toka unapolinunua kunafanya iwe ni moja ya njia mbaya zaidi ya kutumia pesa zako kama hakuna ulazima wa kulimiliki kwakuwa litahitaji ulihudumie kila mara unapolitumia, kuanzia ukarabati, mafuta, bima na vibali vingine.
Watu wenye kipato cha kati wana tatizo sugu la kuishiwa pesa mara kwa mara japokuwa wana kipato cha kila mwezi. Hii ni kwa sababu wengi wanajali zaidi kuwaonesha wenza vitu wanavyomiliki, kama magari – lakini hii inaongeza matumizi ambayo yangeweza kuepukwa na badala yake kufanya maendeleo yenye maana zaidi.