KLABU ya Simba jana imemtambulisha mshambuliaji wake mpya, John Bocco ‘Adebayor’ aliyesajiliwa kutoka Azam FC. Rais wa Simba, Evans Aveva alimkabdhi Bocco jezi ya klabu hiyo ya Dar es Salaam jana, baada kukamilisha taratibu za usajili.
Habari zinasema Bocco ataendelea kulipwa mshahara wa Sh milioni nne kwa mwezi aliokuwa anapata Azam Fc kabla ya mkataba wake kumalizika na kuondoka. Wakati Simba ikimtambulisha Bocco, beki wake, Jamal Mwambeleko aliyejiunga na Wekundu hao wa Msimbazi akitokea Mbao FC ya Mwanza amesema anaitumia Simba kama daraja kucheza soka la kulipwa nje.
Mmoja wa wachezaji walio nje ni Mbwana Samatta anayechezea Genk ya Ubelgiji. Mwambeleko alijiunga na Simba akitokea Mbao FC. Amesema malengo yake ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi ndiyo yaliyomfanya kukubali kutua Simba.
Akizungumzia nafasi yake Simba alisema atapambana kuhakikisha anamshawishi Kocha Joseph Omog ampe nafasi ya kucheza kwani anaamini atatoa ushindani kwa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kwa sababu wote wanacheza beki wa kushoto.
“Mimi ni mchezaji ninayejitambua. nafahamu Simba ni timu kubwa na kazi yangu ni soka, kwa hiyo nimejipanga kuhakikisha najituma mazoezini ili kumshawishi kocha anipe nafasi,” alisema.
Mwambeleko amesajili Simba na kipa Aishi Manula, Yusuph Mlipili, Shomari Kapombe na John Bocco ‘Adebayor’ waliojiunga na Simba kwa ajili ya msimu mpya wa ligi unaotarajiwa kuanza Agosti.
Simba, mabingwa wa Kombe la FA, itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) 2018 ambalo Mwambeleko alisema litamsaidia kutimiza malengo yake. Mbali ya Bocco, wachezaji wengine wa Azam waliokwenda Simba ni kipa Aishi Manula na beki Shomary Kapombe.
Kama ilivyo kwa Bocco anayedaiwa kutia wino kwa mkataba wa Sh milioni 50 na mshahara wa Sh milioni nne, kipa Manula pia anadaiwa kusajiliwa kwa Sh milioni 50.