WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee na Ester Bulaya waliosimishwa kushiriki shughuli za Bunge kwa mwaka mmoja, huenda wakakabiliwa na adhabu zaidi.
Spika wa Bunge, Job Ndugai jana alitoa onyo kuhusu wabunge hao akisema hatua yao ya kuzungumza na kulalamika nje ya Bunge baada ya adhabu yao, haikubaliki na inaweza kuwasababishia adhabu zaidi.
Ndugai alisema kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, chombo hicho kinacho uwezo wa kuita huko waliko, kuwajadili na kuchukua hatua zaidi. “Kuna wenzetu walichukuliwa hatua za kinidhamu na Bunge, lakini wameendelea na malumbano.
Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge tunaweza kuwafuata huko huko waliko na kuwaita kuwajadili na kuchukua hatua zaidi. “Kama unataka kwenda mahakamani si uende, kuna sababu gani ya kuitisha mkutano wa hadhara.
Nawaonya kuhusu hili, kuendelea kuongea vitu huko, tutapambana nao. Ndugu, marafiki na jamaa muendelee kujitahidi,” alisema Spika Ndugai. Wabunge Mdee wa Jimbo la Kawe na Bulaya wa Bunda, waliadhibiwa Juni 5, mwaka huu kwa makosa ya kudharau kiti cha Spika wakati Bunge lilipokuwa likijadili Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.
Mwishoni mwa wiki, Mdee aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa kwamba wanatarajia kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa Bunge. “Nitakwenda mahakamani, wanasheria mbalimbali wameshafika, lakini tunasubiri Mwanasheria Mkuu wa chama ili tuanze mchakato,” alisema Mdee.
Alisema mhimili wa Mahakama uliundwa ili kusimamia haki na kutafsiri sheria. “Mahakama ni chombo pekee kilichoundwa na Katiba ili kusimamia haki, hivyo tunaamini Mahakama itatenda haki,” aliongeza