FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

Chupa 247 za damu zakusanywa Pemba





KITENGO cha damu salama Pemba kimekusanya chupa 247 kati ya 250 walizokusudia kukusanya katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa kitengo hicho, Dk. Abdi Kassim, alisema hayo ni mafanikio makubwa kwa kitengo hicho.
Alisema siku ya maadhimisho ya kuchangia damu, walifanikiwa kukusanya chupa 10, ambazo alisema si kiwango kibaya ambapo wachangiaji wengi walikuwa vijana na klabu za kuchangia damu.
“Katika kipindi hiki sisi tunatoa damu watu asubuhi kuanzia saa 2.00 hadi 5.00, hawa wote wanaokuja ni wanachama wetu waliomo katika klabu zetu za kuchangia damu,”alisema.
Akizungumia changamoto wanazokumbana nazo, alisema ni pamoja na ukosefu wa nyezo za kuwakutanisha wanachama wao.
Akizungumza baada ya kuchangia damu ikiwa ni mara yake ya 48, Abdulla Mohamed Kassim, alisema kuchangia damu ni jambo linalompa faraja kwani anasaidia kuokoa maisha ya wenzake.
“Mimi najisikia faraja kuona nachangia damu kusaidia kuokoa maisha ya wenzangu ambao hawana sehemu ya kupata huduma ya damu pale wanapohitaji,” alisema.
Aliiomba serikali kuweka mazingira rafiki katika sehemu ambazo watu wanachangia damu, ili wachangiaji hao waweze kuvutika zaidi.