MECHI ya Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara kati ya watani wa jadi, Yanga na Simba iliyokuwa ichezwe Oktoba 14, 2017 sasa imesogezwa mbele hadi Oktoba 28, 2017.
Mabadiliko hayo yaliyofanywa na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) na kuridhiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) yalitangazwa jana na TFF iliyotoa ratiba mpya ya ligi. Mbali ya kubadilishwa tarehe, bodi pia imebadilisha mwenyeji wa mechi ambapo sasa Yanga itakuwa mwenyeji wa mechi ya kwanza na Simba mechi ya marudiano.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, mechi hiyo sasa itachezwa uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam badala ya Taifa na tarahe ya mechi ya marudiano itapangwa baadaye. Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema mchezo wa Simba na Yanga umesogezwa mbele kwa siku 14 katika raundi ya nane ambapo usajili wa dirisha dogo unatarajiwa kufunguliwa Novemba 15 na kufungwa Desemba 15 mwaka huu “Ratiba imebadilika kwa kiasi kikubwa.
Kwa mujibu wa ratiba ya awali ligi ilikuwa imalizike Mei 5, 2018 lakini sasa itamalizika Mei 28, 2018,” alisema Lucas. Pia Lucas alisema raundi ya pili itaanza Januari 19, 2018 badala ya Desemba 30, 2017 kama ratiba ya awali ilivyoonesha.
Baada ya michezo ya Agosti 26 na 27, Ligi Kuu ya sasa itaendelea Septemba 9 na 10 kwa michezo minane viwanja tofauti. TFF iliunda kikosi kazi kupitia ratiba hiyo baada ya awali kusababisha ligi isimame baada ya mechi ya kwanza tu kupisha mechi za kimataifa za Taifa Stars Kwa mujibu wa ratiba hiyo, awamu ya pili timu hizo zitakutana katika raundi ya 23 ambayo itaanza Machi 14, 2018.
Awali zilikuwa zikutane Machi 3, 2018 Pazia la ligi linatarajiwa kufungwa Mei 26, ambapo Simba itamaliza ugenini kwa kucheza na Majimaji na Yanga itamaliza nyumbani kwa kucheza na Azam FC.