SASA ni dhahiri kwamba tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa mkombozi wa afya za Watanzania na raia wa nchi za Afrika Mashariki na Kati kutokana na kasi yake ya kuokoa maisha ya watu wengi, tena kwa gharama nafuu.
Hali hiyo ni tofauti na miakamichache iliyopita ambapo serikali ililazimika kuwapeleka wagonjwa wengi wa moyo nje ya nchi, hususani India, tena kwa gharama kubwa zilizokuwa zinaiumiza nchi. Kuanzishwa kwa hospitali hiyo ya moyo ya kisasa na ya kipekee katika ukanda huu, kumeonekana kuzaa matunda, kwani mbali ya kusaidia wengi kupata tiba kwa wakati, tena kwa gharama nafuu, serikali imeokoa zaidi ya Sh bilioni 45 baada ya kuacha kupelekwa wagonjwa nje ya nchi kwa kiwango cha asilimia 85.
Hayo yalithibitishwa hivi karibuni na daktari bingwa wa moyo nchini ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya JKCI, Profesa Mohamed Janabi (pichani). Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, alisema tangu mwaka 2015, takribani wagonjwa 1,500 wa moyo wamefanyiwa upasuaji wa moyo kwa kupasua kifua, kuzibua mishipa ya moyo, upasuaji wa mishipa ya damu, kuweka vyuma ndani ya moyo, kuweka betri (pacemarker) na kadhalika.
Hii ina maana kwamba, kwa idadi hiyo ya wagonjwa, serikali imeokoa zaidi ya Sh bilioni 45, kwani kwa kila mgonjwa aliyekuwa anapelekwa nje ya nchi, alikuwa analipiwa kiasi cha Sh milioni 30 za kuanzia matibabu, wengi wakiwa waliokuwa wanapelekwa kwa tiba ya muda mfupi ya wiki hadi siku 10 na gharama ikiongezeka kwa wale wanaolazwa na kubaki India kwa muda mrefu.
“Tiba ya moyo ya ghali sana, sasa kwa hawa wa nje nimechukuliwa hicho ni kiwango cha chini cha kuanzia, lakini gharama huenda hadi Sh milioni 100 kwa mgonjwa, sasa unaweza kuona ni kwa jinsi gani serikali ilikuwa inatumia fedha nyingi kutibu Watanzania. “Lakini sasa tumejikomboa, tunaokoa maisha ya watu wetu hapa hapa nyumbani, kwa idadi kubwa, uhakika na kwa gharama nafuu sana. Pesa ambayo wakati ule ingetumika kupeleka mgonjwa mmoja nje ya nchi sasa inaweza kutibu watu watano hadi 10 kutegemea na tatizo la mgonjwa,” alisema Profesa Janabi.
Aliongeza kuwa, anajivunia kuiongoza taasisi hiyo, lakini kikubwa ni mafanikio ya haraka kama yalivyokuwa matarajio ya Serikali, huku sasa ikigeuka pia kuwa kimbilio la wagonjwa kutoka nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Awali, wagonjwa ya moyo walishika nafasi ya pili kwa kupelekwa kutibiwa nje ya nchi, wakitanguliwa na wale wa saratani. Magonjwa kama figo ndiyo yaliyofuatia baada ya moyo.
Anasema kwa sasa kutokana na huduma za ubora wa kimataifa zinazotolewa na taasisi yake, mbali ya kuwa tumaini jipya kwa wagonjwa wa moyo nchini, lakini pia inategemewa na nchi jirani ambazo zimeanza kupishana kuleta wagonjwa wake nchini. Si wagonjwa tu, bali pia imekuwa ikipokea madaktari kutoka nje ya nchi (Uganda, Sudan Kusini, Ethiopia) wanaoletwa na nchi zao kuja kujifunza zaidi juu ya utaalamu wa magonjwa ya moyo.
“Tumekuwa darasa la kufundishia upasuaji wa moyo Afrika ndiyo maana tunapokea madaktari kutoka nchi mbalimbali, lakini pia tumekuwa tukienda kutoa huduma nje ya nchi, mathalani tumeshafanya hivyo Rwanda ambako tulipeleka wataalamu wetu kufanyia upasuaji wagonjwa 25 mwaka jana 2016. “Tumeshafikiria kuomba rasmi kuwa na chuo cha matibabu ya moyo (chuo shirikishi na MUHAS), hivyo nasi JKCI tutaanza kutoa mafunzo kwa wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali Afrika Mashariki na Kati.
Hapa ndipo madaktari wa upasuaji wa moyo watakuja kupata utaalamu wa upasuaji hadi kwa ngazi ya shahada ya Uzamili katika masuala ya moyo. “Ukiondoa madaktari, wauguzi, mafundi na wafanyakazi wa kada nyingine, pia wagonjwa wanamiminika kutoka Kenya, Comoro, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na sasa tunategemea kuwapokea kutoka Malawi na Zambia,” alisema Profesa Janabi anayejivunia taasisi yake kuwa na vifaa vya kisasa, ukiwemo mtambo mkubwa kabisa na wa kipekee Afrika Mashariki na Kati wa kuzibua mishipa ya moyo na ya damu iliyoziba, Catheterization Laboratory (Cath Lab) ambao uliigharimu serikali kiasi cha Sh bilioni 4.5 uliponunuliwa mwaka 2013.
Kupatikana kwa mtambo huo na jengo la kisasa la taasisi lenye uwezo wa kulaza wagonjwa 128 kwa wakati mmoja, 15 wakiwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU), kumeifanya taasisi kuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa wengi zaidi tofauti na miaka ya nyuma ilipokuwa inahudumia wastani wa wagonjwa 50 tu wa upasuaji kwa mwaka. Kwa sasa, ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 100 mpaka 200 kwa siku wanaopata huduma bila kulazwa.
MALENGO YA JKCI
Akizungumzia malengo ya taasisi hiyo, alisema kwa mwaka huu, wanakusudia kufanya upasuaji wa bila kufungua kifua kwa wagonjwa zaidi ya 1,000 tofauti na 650 wa mwaka jana, wakati katika upasuaji wa vifua, lengo ni kuhudumia wagonjwa 400 tofauti na 353 wa mwaka jana. Alisema hata hivyo, wanajivunia kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wametibiwa na wataalamu wazawa, huku asilimia 30 pekee ndiyo waliotibiwa na madaktari wanaotoka nje ambao huja kwa makundi kumi kila mwaka kutoka nchi na mabara tofauti duniani zikiwemo Marekani, Ulaya, Israel, Australia, India na Falme za Kiarabu.
“Wataalamu wetu wanafanya kazi kubwa na nzuri, kwa kiwango cha kimataifa… hatuna rekodi ya vifo vingi, kwa mfano katika kupasua kifua, tuna asilimia 7.5 tu vifo, ni matarajio yetu kuishusha zaidi kuwa chini ya asilimia 5, kati ya viwango vya kimataifa vya asilimia 13, hapo kwenye kuzibua mishipa vifo ni chini ya asilimia moja. “Ukiangalia hili ni jambo la kujivunia mno. Taasisi imekuja kwa wakati mwafaka, kwani kote duniani magonjwa ya moyo ambayo si ya kuambukiza yanazidi kama ilivyo kwa figo, kisukari na kadhalika… ni ukombozi kwa Watanzania na majirani zetu ambao nao walikuwa wanahangaika kupeleka wagonjwa India na kwingineko kwa gharama kubwa.
“Tumeokoa na tunalenga kuokoa maisha ya wengi ambao zamani walipokuwa wakifariki kutokana na matatizo haya tulikuwa tunasema ‘ni kazi ya Mungu,’ lakini kwa sasa wengi wanapata tiba na msaada wa kitaalamu,” alisema. Alitumia fursa hiyo kuzitaka nchi za Afrika Mashariki na Kati kuitumia Taasisi ya JKCI kwani pamoja na kuwa na gharama nafuu, lakini pia inapatikana katika mazingira yanayoshabihiana kwa mila na desturi, lugha, vyakula na kadhalika.
KUANZISHWA KWA TAASISI
Ameshukuru wazo la kuanzisha taasisi hiyo, hasa nguvu kubwa iliyofanywa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ya kupigania kuanzishwa kwa taasisi hiyo. “Wazo la kuwa na hospitali ya moyo lilianza tangu awamu ya kwanza, wataalamu wawili walipelekwa nje kusomea masuala ya moyo, Profesa Mtulia (Idrissa) na Profesa Mahalu (William), lakini baada ya kurejea lengo halikutimia kwa sababu miundombinu ilikuwa hajawa tayari, hata mmoja wa madaktari wa Nyerere (Dk William Makene) alikuwa mtaalamu wa moyo.
Hivyo nia ya serikali ilitaka kuwa na hiki kitu siku nyingi, lakini ndoto zimekuja kutimia katika awamu ya nne na kuendelezwa na awamu hii ya tano,” anakumbuka. Anaongeza kuwa, Rais mstaafu Kikwete alianza kutimiza ndoto za Nyerere kwa kupeleka wataalamu kutoka nchini 26 kwenda India mwaka 2005/06 na waliporejea mwaka 2008, walianza kazi kwa kutumia vitanda vinne tu vilivyoombwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na pia nafasi ya kulazwa wagonjwa katika Wodi Namba 12 ya Kibasila, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Lakini mambo yalibadilika baada ya ombi la Rais Kikwete kwa Serikali ya China ya kuomba kusaidiwa kufanikisha kuwa na hospitali ya moyo kukubaliwa, hivyo China ikachukua jukumu la kujenga jengo la sasa kwa gharama ya Sh bilioni 13. 6, huku serikali ikitoa Sh bilioni 13 kwa ajili ya mashine za kisasa vitanda na vitu vingine muhimu, hivyo kuanza rasmi kazi ikiwa na sura ya sasa mnamo Septemba 5, 2015.
CHANGAMOTO
Kutokana na shughuli za taasisi hiyo kupokelewa kwa haraka, imekuwa ikipokea wagonjwa wengi kiasi cha kuanza kuona nafasi iliyopo ni ndogo, hivyo kuiomba serikali nafasi nyingine. “Kwa Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara labda tunazidiwa na Angola na Namibia tu kwa sababu walianza mapema na wanapokea misaada mingi kutoka Portugal.
Nasi tuendako, naamini ndani ya miaka mitano tutakuwa bora zaidi, kumbuka kwa sasa tupo katika tano bora kwa upande wa taasisi za umma, zipo za binafsi Afrika Kusini zinazoongoza, lakini tunaelekea kwenye ubora zaidi,” alisema Profesa Janabi. HUDUMA KWA WAJAWAZITO Mbali ya huduma za upasuaji wa moyo, kuzibua mishipa na nyinginezo, alisema taasisi hiyo pia inatoa huduma nyingine, ikiwemo ya kipimo kinachojulikana kwa jina la Fetal Echo, maalumu cha kuwapima wajawazito ili kuangalia endapo mtoto aliyeko tumboni analo tatizo la moyo.
“Tunahamasisha kina mama wajawazito waje kupima kwani itasaidia kujua mapema endapo mtoto ana tundu la moyo na hivyo kabla hajazaliwa tunakuwa tumeshaandaa matibabu yake,” alisema. Hata hivyo, alisema mwamko ni mdogo na akawataka wajawazito kujitokeza ili kuepuka kujifungua watoto wenye matatizo ya moyo.
“Kipimo hiki ni kama kilivyo kile cha Ultra Sound, hakina mionzi wala madhara yoyote kwa mjamzito endapo atapimwa, tunaendelea kuwaelimisha wajawazito waje wafanyiwe kipimo hiki kwa ajili ya usalama na afya kwa watoto wanaotarajia kujifungua,” alisema na kuongeza kuwa, takwimu zinaonesha kuwa kati ya watoto milioni moja wanaozaliwa Tanzania kwa mwaka, asilimia moja watakuwa na tatizo moja au lingine la moyo.