FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

Malinzi, makamu wake wavaana urais wa TFF





UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) umezidi kunoga baada ya makamu wa rais, Wallace Karia kujitosa kumpinga bosi wake, Jamal Malinzi kuwania urais.
Karia alikuwa makamu wa rais chini ya Malinzi katika uongozi unaomaliza muda wake mwaka huu, kabla ya hapo alikuwa mwenyekiti wa bodi wa Ligi chini ya uongozi wa Leodegar Tenga.
Mwingine aliyechukua fomu kuwania urais ni Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Iman Madega. Uchaguzi wa TFF unatarajiwa kufanyika Agosti 12 mwaka huu mjini Dodoma. Aidha, mjumbe wa kamati ya utendaji ya TFF, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ naye alimejitosa kuwania nafasi ya makamu wa rais akichuana na Katibu Mkuu wa zamani wa iliyokuwa FAT, Michael Wambura.
Aidha, wabunge watatu wamejitosa kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi huo utakaofanyika Dodoma. Wabunge hao ni Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu Tabora, John Kadutu, Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo na Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, Musa Sima, ambao kwa nyakati tofauti walifika katika ofisi za TFF Dar es Salaam kuchukua fomu na kueleza sababu zilizowasukuma kujitosa.
Akizungumza na gazeti hili Kadutu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Tabora (TAREFA) alisema yeye kama mwanamichezo ameamua kujitosa ili kusaidia kurudisha enzi za soka la Kigoma na Tabora.
“Zamani mikoa ya Tabora na Kigoma ilikuwa maarufu kwa kutoa wanasoka bora lakini sasa ni tofauti kwa sababu viongozi wamesahau majukumu ya kusaidia kukuza soka,” alisema Kadutu.
Naye Nyongo ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Simiyu alisema ameamua kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho ili kuleta mabadiliko katika soka kupitia kanda ya Simiyu na Shinyanga.
“Mimi ni mwanasiasa lakini katika siasa kuna michezo, kwenye dini kuna michezo, hivyo ni wakati wangu kusaidia mpira usonge mbele ili kushindana kimataifa,” alisema Nyongo.
Naye Sima ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Singida anayegombea kupitia kanda ya Singida na Dodoma alichukuliwa fomu yake na Nyongo. Wajumbe wengine ambao walichukua fomu jana ni Ayoub Nyenzi (Iringa na Njombe) na Khalid Abdallah (Tanga na Kilimanjaro).