FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

B ANNA, SAKAYA WAFURAHIA BULAYA, MDEE KUTIMULIWA BUNGE



                                                   

MHADHIRI Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Banna, amesema adhabu iliyotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee na Ester Bulaya ya kufungiwa shughuli za Bunge kwa takriban mwaka mmoja ni sahihi.

Wabunge hao walipewa adhabu hiyo juzi kwa kosa la utovu wa nidhamu katika kikao cha Bunge na kukidharau Kiti cha Spika, Ijumaa iliyopita. Wabunge hao walionesha utovu huo wa nidhamu bungeni, wakipinga Mbunge wa Kibamba, John Mnyika kutolewa nje ya Bunge kwa agizo la Spika wa Bunge Job Ndugai.

Kutokana na Mnyika kukaidi amri ya Spika ya kumtaka akae huku Mnyika akitaka ombi lake la utaratibu bila kujali maelekezo ya Spika, Ndugai aliagiza askari kumtoa nje ya Bunge na kutohudhuria vikao vya Bunge kwa wiki moja.
Wakati askari wakimtoa Mnyika ukumbini, Halima ambaye ni mbunge wa Kawe na Bulaya wa Jimbo la Bunda Mjini, waliinuka katika viti vyao na kuelekea upande wa askari waliokuwa wakimtoa nje Mnyika huku Bulaya akihamasisha wabunge wengine wa upinzani kuondoka na kususa Bunge.

Kutokana na hali hiyo, Ndugai aliiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kujadili adhabu mwafaka na ndipo baada ya mjadala, Bunge likaridhia wabunge hao kutoshiriki shughuli za Bunge vikiwamo vikao vya Bunge na safari na vikao vya Kamati za Kudumu hadi mwezi Aprili mwakani katika Bunge la Bajeti mwaka 2018/ 2019.

Akizungumza na gazeti hili, Dk Banna alisema wabunge hao walidhalilisha Bunge, wapiga kura na wananchi katika majimbo yao. Alisema wabunge wanapaswa kuheshimu kanuni za Bunge na kuzifuata ili kufanya uwakilishi mzuri kwa wananchi.

“Kuna gharama ya kuwa Mheshimiwa na hiyo ni kuwa na hekima kwa kuwa chochote kinyume na hapo ni kosa tena kubwa na wabunge hao wamevuna kile walichokipanda,” alisema.

Mbunge wa Kaliua wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya alisema kuwa adhabu hiyo ni mwafaka kwa wabunge hao kutokana na kuwa walikwishaonywa. Alisema, Bunge linatakiwa kuheshimiwa na wabunge hao wamekuwa watata mara kwa mara katika kufuata kanuni zilizowekwa.
Alisema, wabunge wanatakiwa kuwa na nidhamu, uvumilivu na hekima ya hali ya juu kipindi chote wakati Bunge likiwa linaendelea. Alisema kwa upande wa Mdee, ndani ya kipindi kifupi amefanya makosa kadhaa ya utovu wa nidhamu.
Alisema, mbunge huyo aliitwa kwenye kikao cha Kamati ya Nidhamu mwezi Aprili baada ya kudaiwa kumtukana Spika Ndugai na alipewa karipio kali la kumtaka asirudie kosa. Alisema wakati wakiwa kwenye kikao hicho, aliambiwa wazi kuwa iwapo atarudia tena kosa, atapewa adhabu kali zaidi na kwa sasa anatumikia kile alichoonywa.

Kutetea wezi wa madini Wakati huo huo, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde amesema kufukuzwa bungeni kwa wabunge wa Upinzani, kumetokana na kutetea wezi wa madini kwani wamekuwa wakipinga juhudi za Rais John Magufuli katika kuokoa rasilimali za Taifa yakiwamo madini.
Akizungumza kwenye Viwanja vya Bunge jana, mbunge huyo wa CCM alisema, “Mimi ndio nilikuwa nachangia na hili jambo la mchanga wa dhahabu lilikuwa linazungumziwa kipindi cha nyuma.
“Mwongozo wa Mnyika alisimama kama anatetea wezi wa mchanga wa dhahabu watu wasifikiri kuwa kuna mtu ameonewa, lakini hoja ya kutetea wezi wa dhahabu ndiyo imemgharimu Mnyika.”

Aliongeza Lusinde, “Tunajiuliza maswali ni kwabnini watu hawa walikuwa wanapinga wizi kipindi cha nyuma, lakini sasa wanatetea kuna nini kimetokea hapo katikati? “Kwa nini wanatetea wezi? Rais John Magufuli amejitahidi kuokoa madini ili fedha zitusaidie katika huduma zingine, lakini wabunge wanapinga.”

Naye Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi (CCM) alisema, “Tulikuwa tunajadili mchanga wa dhahabu sasa tunapongeza hatua alizochukua rais, lakini watu ambao walikuwa wanazungumzia suala hilo kwa miaka mingi wanaanza kupinga, hapa lazima tuhisi kuwa kuna kitu huenda wamepewa na hao wezi.”

Alieleza kuwa haiingii akilini kwa wabunge ambao ni wazalendo kupinga juhudi zinazofanywa na Rais kama hawajapewa fedha yoyote na hao waliokuwa wanaliibia taifa. “Ifike mahala tuseme ukweli katika hili uzalendo ulitakiwa kwani tuliibiwa taifa na hiki ndicho kimefanya Mnyika aadhibiwe kwa kuwa alitetea wezi na ndicho chanzo na mbunge mwingine kuropoka kuwa ni mwizi kwa sababu haeleweki,” alieleza Chumi.

Alisema hata adhabu waliopewa wabunge Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda Mjini), chanzo chake ni kumtetea John Mnyika aliyekuwa anatetea wizi unaofanywa na kampuni za madini, jambo ambalo halikubaliki na kuwaomba wabunge kuungana katika kushughulikia mambo ya kitaifa.
Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) alisema wabunge hao wa Upinzani wanapaswa kuheshimu mamlaka inayoongoza Bunge. “Waache waende. Pale bungeni kuna viongozi wetu, ni lazima kuwaheshimu. Kuheshimu mamlaka ni muhimu na ni lazima,” alieleza Naibu Waziri huyo wa zamani.
Juzi, Bunge kwa pamoja, lilipitisha adhabu ya kusimamishwa kwa mikutano mitatu wabunge wa Chadema, Mdee na Bulaya kutokana na utovu wa nidhamu na kutoheshimu mamlaka ya Spika.

Hawatahudhuria mikutano ya Bunge kuanzia juzi katika Mkutano wa Saba unaoendelea, Mkutano wa Nane mwezi Novemba na ule wa Tisa Februari mwakani. Watarejea bungeni Aprili mwakani wakati wa Mkutano wa Bunge la Bajeti, na muda wote huo hawataruhusiwa kushiriki shughuli zozote za kibunge.

Kiini cha kufungiwa kwao ni vurugu zilizotokea wakati Lusinde akichangia Bajeti ya Nishati na Madini, ambako alikatizwa na Mnyika aliyekuwa akitaka Spika achukue hatua dhidi ya mbunge aliyedai amemwita mwizi.

Katika hotuba yake ya Kambi ya Upinzani kwa bajeti hiyo, Mnyika alipinga ripoti ya Kamati ya Rais Magufuli ya uchunguzi wa makinikia, kiasi cha wabunge wengine kuhoji upinzani wana ajenda gani na kueleza kuwa wanatumiwa na waliofilisi nchini katika sekta ya madini.