FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

Bila Manji umaskini Yanga hauwezi kuondoka?








MEI mwaka huu, Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji aliandika barua ya kujiuzulu nafasi yake baada ya kuiongoza klabu hiyo kongwe na moja ya klabu kubwa mbili nchini kwa miaka 11.
Uamuzi huo wa Manji umekuja miezi michache baada ya mwishoni mwa mwaka jana kuikodisha klabu hiyo kwa miaka 10, uamuzi uliofikiwa kwenye mkutano mkuu wa wanachama wa klabu hiyo. Katika hatua hiyo ya kuikodisha Yanga, Manji ilikuwa achukue asilimia 75 na asilimia 25 ziingie kwa klabu kwa miaka hiyo 10. Tayari Manji alifanya taratibu zote na kusajili kampuni ya Yanga Yetu ambayo ndiyo ingekuwa ikimiliki nembo na jina la Yanga kwa miaka 10.
Hata hivyo, jambo hilo halikufanikiwa baada ya Serikali kuingilia kati na kutaka uwepo utaratibu unaoeleweka wa namna ya kuiendesha klabu hiyo. Kujiuzulu kwa Manji sio jambo geni. Kwa miaka yake 11 mara kadhaa amekuwa akitishia kujiuzulu na kisha anarudi tena madarakani muda mfupi baada ya kuombwa kufanya hivyo na baadhi ya wazee wa klabu na wanachama kutokana na shinikizo. Huwa kama mchezo wa kuigizia hivi.
Chini ya Manji, Yanga imekuwa ikifanya vizuri kwenye michuano ya ndani kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya soka ya Vodacom Tanzania bara na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa licha ya kwamba haifiki mbali kwa kiasi kile kinachotamaniwa na Watanzania wengi wapenda soka. Msimu uliopita ilifika hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la Shirikisho Afrika, msimu huu haikufua dafu ilirudia yale yale ya siku zote kwa timu za Tanzania kwenye michuano ya kimataifa.
Je, Yanga inamhitaji Manji? Miaka ya nyuma, iliaminika kwamba tajiri huyo ndiye aliyekuwa uti wa mgongo wa mafanikio ya Yanga, kwamba akiondoka, Yanga haiwezi kufika popote. Kadri siku zinavyoenda, jambo hilo linaonekana si sahihi kwani uzoefu wa muda mrefu unaonesha kuwa, Yanga iliwahi kuongozwa na mashabiki na viongozi wasio matajiri lakini ilifanya vizuri na hilo linadhihirika kwenye idadi ya makombe ya Ligi Kuu iliyotwaa kwani ndiyo timu pekee iliyobeba taji hilo mara nyingi nchini.
Sijajua bado sababu ya wanachama na mashabiki wa Yanga kuamini Yanga haiwezi kwenda bila ya Manji kiasi cha kila anaposema anajiuzulu, kukosa mbadala na kwenda kumwangukia arudi. Sidhani kama wanachama wa Yanga wamejiuliza wanakosa nafasi ngapi kutoka kwa wafadhili wengine.
Wanachama wa Yanga walipaswa kujiuliza mapema kwa miaka yote hii kuwa inakuwaje klabu yao ishindwe kujitegemea wakati ni kubwa, yenye wanachama wengi na mashabiki lukuki nchi nzima na hata nje ya nchi kama ilivyo kwa klabu nyingine kongwe kama mpinzani wao, Simba na za Ulaya.
Iweje basi, kwa muda wote huo wakubali kuweka mayai kwenye kikapu kimoja cha kumtegemea mtu mmoja tu, ambaye hata pale anapoona anaelemewa na mzigo wa uongozi na kuomba kuondoka, wanamzuia na hivyo kufanya wafadhili wengine wenye nia ya kuingia washindwe kufanya hivyo. Chini ya Manji, Yanga imeendelea kuwa tegemezi mno, haiwezi hata kulaza wachezaji wake kwenye hoteli nzuri, haiwezi kulipa mishahara ya wachezaji, haiwezi kusafirisha timu, inawezekana vipi?.
Wakati kiongozi akiwa Tabu Mangala hali ilikuwaje? Ngozoma Matunda je?, Tarimba Abbas?, George Mpondela, Francis Kifukwe? Imani Madega je? Hao ni kati ya viongozi waliongoza Yanga bila ukwasi. Hata hivyo, pamoja na kutokuwa na ukwasi, viongozi hao waliondoka wakiwa wameacha rekodi za kuipa Yanga mataji mbalimbali achilia mbali kufanikisha timu hiyo kucheza michuano ya kimataifa. Hawa walifanya haya bila kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha.
Enzi zao, pamoja na changamoto zote, haikutokea wachezaji kugoma kisa kudai stahiki zao, haikutokea timu kukosa nauli ya kutoka sehemu moja kwende nyingine. Mara zote wanachama, wafadhili na watu wenye mapenzi mema na Yanga, walisaidia kuokoa jahazi kuonesha Yanga ilivyo na hazina. Kwa miaka 11 aliyokaa Yanga, Manji hajafanikiwa kutimiza ndoto yake ya kuijengea uwanja mpya Yanga achilia mbali ule wa nyasi bandia pale Kaunda.
Hii inaonesha kuwa ni vigumu kwa mtu kutimiza matarajio yote kwa timu kubwa kama Yanga hata kama mtu angekuwa na ukwasi ulioje. Ni kutokana na hilo, kuna haja kwa wana Yanga kumsaidia Mwenyekiti wao, Manji anapoomba ajiuzulu, wamkubalie ili watu wengine wenye uwezo kama wake au chini ya hapo au zaidi, nao watoe mchango wao kwani timu za Yanga na Simba zimekuwa za umma ambapo kila mtu huchangia nguvu zake na pale anapoona anaelemewa, huomba wengine wampokee kijiti kama anavyoomba.
Yanga hadi sasa imeendelea kutumia uwanja wake wa Kaunda kwa mazoezi licha ya kuwa, uwanja huo uliojengwa miaka ya 70 jengo lake lilipojengwa, hali inayokosesha wachezaji mazoezi mazuri. Ni wajibu wa wana Yanga kumsikiliza Mwenyekiti wao anapowaomba aachie ngazi ili hatimaye mipango mingine kama ya kukarabati kiwanja hicho au hata kujenga kingine kipya iliyokwama, iweze kuendelezwa na watu wengine au hata kwa msaada wa Serikali kuendeleza alipoishia yeye.
Ni ukweli usiopingika kuwa Manji ameifanyia Yanga mambo mengi makubwa na mazuri kama vile walivyowahi kufanya wafadhili wengine wakubwa wa zamani wa Yanga, Abbas Gulamali, Mohammed Virani, Muhsin Hassanali na kina Mangara na Mzee Abeid Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar. Hao kwa kushirikiana na wanachama wa wakati huo waliifikisha Yanga pale alipoikuta yeye na kuiendeleza hadi ilipo akishirikiana na viongozi wengine wakikabili changamoto mbalimbali.
Lakini kwa kuwa chagamoto siku zote haziishi na kwa kuzingatia kuwa hivi sasa mwenyekiti ana majukumu mengine makubwa ya kisiasa akiwa Diwani wa Mbagala (CCM), ingekuwa jambo la busara wana Yanga wakakubali kuachia kwake ngazi ili aweze kuwajibika kwa nafasi nyingine. Kama ataondoka, bado Manji atakuwa na nafasi kubwa ya kutoa mchango wake kwa Yanga, timu anayoipenda akiwa mwanachama wa kawaida na pia kiongozi mstaafu lakini zaidi kama mfadhili kama akipenda kwani ana makampuni kadhaa ambayo yanaidhamini Yanga na yanaweza kuendelea.
Suala linalogomba pengine ni lile la wanachama wa Yanga kuaminishwa na kukubali kuwa, bila Manji Yanga haiwezi kwenda, Yanga haiwezi kusimama, Yanga haiwezi kushindana na Simba. Hawa wanatakiwa kuelimishwa kidogo kuwa Yanga ilikuwapo kabla ya Manji na pia itaendelea kuwepo baada ya yeye kama ambavyo walipita kina Mangala, Karume, Madega, Tarimba n.k.
Na uhalisia ni kuwa, wakati mwingine mtu akitoka, anapata muda mzuri wa kutafakari na kuja na mipango mipya ya kusaidia sekta ya michezo kama alivyofanya Tarimba ambaye amerudi kwenye soka akiwa ameleta udhamini wa michuano ya Sportpesa inayoshirikisha timu za Yanga na Simba. Jambo moja ambalo wana Yanga wanapaswa kulikubali ni kuwa Mwenyekiti wao, Manji ni mtu mwenye shughuli nyingi na hivyo wanapaswa kumwelewa anapowaomba apumzike kidogo.
Badala ya kuendelea kumsumbua arudi, wanapaswa kuangalia mbele jinsi ya kuendesha Klabu yao bila yeye na kama inalazimu sana, waombe ushauri wake kwa masuala ya kibiashara ambayo yanaweza kuwasaidia kwani ni mmoja wa wafanyabiashara wenye mafanikio makubwa nchini. Kwa hili la kuombwa mchango wa mawazo, Manji hatashindwa kuendelea kuwashauri Yanga huku akiendelea kuangalia viongozi wengine wa kuchaguliwa wanavyoisimamia na kuendesha klabu.
Wasipofanya hivyo, iko hatari kwa timu kushindwa kupiga hatua zaidi za kimaendeleo kwa kubaki ikimsihi mtu mmoja ambaye kwa mtazamo wake, anahitaji kupumzika ili wengine watoe mchango. Hadi kuamua kutangaza kuwa anajiuzulu, Manji atakuwa alikuwa amefanya mawasiliano na kupata ushauri wa watu wengi, wakiwemo wanachama, viongozi wenzake hivyo ni vigumu kuamini kuwa, yale wanayomwambia wanachama, umuhimu wake kwa Yanga kuwa hayajui na anayasikia sasa.
Kama ni hivyo, hii ina maana kuwa, uamuzi wake umelenga kuwapa wana Yanga, fursa adhimu ya kupata watu wengine wa kuiongoza na kuisaidia kifedha timu yao na kwa ujio wa SportPesa ni dalili njema kuwa, inawezekana kuwa wako wengi zaidi wanaoweza kuja kuwekeza kama ataondoka. Pamoja na ndoto za kuifanya Yanga iwe kama TP Mazembe, Yanga ina wajibu wa kutafakari aina ya program zao kama zimelenga kufika huko na viongozi kama wana uwezo wa kuwafikisha huko.
Mazembe si ya mtu mmoja, hata rais wake, Moise Katumbi alipokuwa na matatizo na serikali yake, haikuwahi kusikika wachezaji wamekwama kulipwa stahili zao, ni kwa sababu timu haikuwa ya mtu mmoja, mambo mengine yanakwenda hata kama bosi ana matatizo. Yanga ilikuwa Manji akiumwa, akisafiri basi wao wapo taabuni. Huu ni wakati wao wa kutafakari hatma ya timu yao bila Manji.
Azam Media imenunua haki za kurusha matangazo ya mechi za Ligi Kuu, kila timu ikipewa sh milioni 100, Yanga walikataa wakidai fedha ni chache na wao ni klabu kubwa. Je, wangepoteza nini kama wangezipokea na kuongezea kwenye bajeti yao na kutafuta wadhamini zao wa kuwasaidia? Matokeo yake kila mmoja alishuhudia, baada ya Manji kukaa pembeni, viongozi wa Yanga walivyohaha kuzifuatilia fedha hizo. Si vyema hata kidogo kwa Yanga kuendelea kuwa ombaomba.
Yanga hivi sasa inatakari kuhusu fedha za usajili. Ni wazi ingekuwa na msimamo kuhusu mapato yake, usajili usingekuwa tatizo. Wapo wanaodai chini ya Manji wachezaji walilipwa mishahara mizuri. Ni kweli, lakini zama za sasa si kama zile za kina Mangala, Matunda, Kifukwe na Tarimba. Maisha ya sasa yamebadilika, hivyo ni lazima kiwango cha mshahara wa wachezaji kitabadilika, ni wajibu wa viongozi kuboresha maslahi ya wachezaji wa klabu yake bila kujali ukata au ukwasi.
Viongozi Yanga hawakuwa na sababu ya kuzikataa fedha za Azam hasa kwa vile hali ya klabu zetu inajulikana. Dawa ilikuwa kuzikubali kisha kutoa pendekezo nini kifanyike. Miaka ya nyuma hata Sh milioni 10 haikuwa ikipatikana kwa timu shiriki kwenye ligi, hiyo ni hatua kubwa imepigwa. Katikati ya msimu uliopita, Yanga na Simba zilimaliza mikataba yao na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na kampuni hiyo haikuongeza tena mkataba.
Hapo ndipo timu hizo kongwe zilipohaha zaidi, maana zile fedha kidogo za kulipa mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi zikawa hazipatikani. Lakini hilo tisa, 10 ni kitendo cha Yanga kukosa basi, maana sasa baada ya TBL kutoongeza mkataba, Yanga bado ikaendelea kulitumia basi lenye nembo ya waliokuwa wafadhili wao. Ni wakati muafaka kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu kumiliki basi lao sasa, lakini si hivyo.
Hadi Manji anatangaza kujiweka pembeni Yanga, anaidai zaidi ya sh bilioni tano, ina maana, kama hatarudi kama ilivyo kawaida yake ya kujiuzulu na kurudi, Yanga itapaswa kulipa hilo deni. Swali italilipaje. Kama inaweza kukopeshwa na Manji na kulipa, vipi isikope kwa mwingine na kulipa. Ninavyoona, ni heri Manji alivyokaa pembeni.
Huu ndio wakati wa viongozi wengine waliobaki kuonesha kuwa, hakuomba uongozi kwa kivuli cha mtu bali walisimama wenyewe kwa uwezo wao. Viongozi waliobaki waoneshe kuwa wanaweza kuiongoza Yanga kama ilivyo, maskini lakini inayoweza kusimama yenyewe na kusaidiwa na kila mtu kadri ya uwezo wake na kuheshimu michango ya watu kama Manji na kuwaenzi wanapochoka na kuomba kupumzika salama.