FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

JPM amtwisha Jaji Mkuu vita dhidi ya rushwa


RAIS John Magufuli amemtaka Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kuhakikisha vyombo vya Mahakama vinashughulikia ipasavyo kesi zote za rushwa na ufi sadi nchini.
Aidha, amefichua siri ya kumteua Profesa Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu Januari 18, mwaka huu, akieleza kuwa alichukua hatua hiyo, kwa kuwa hakuwa na historia ya kutosha kuhusu sifa za majaji waliopo nchini. Lakini sasa ameridhishwa na uwezo wake na kumpa nafasi hiyo. Pamoja na hayo, kwa upande wake, Jaji Juma, ameanika mikakati yake ya kuboresha sekta ya Mahakama nchini ikiwa ni pamoja na kuboresha majengo ya mahakama nchi nzima na kuanza kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na uendeshwaji na utolewaji maamuzi ya kesi kwa uwazi.
Akizungumza Ikulu Dar es Salaam jana katika hafla ya kumuapisha rasmi Jaji Profesa Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Dk Magufuli alisema kazi ya Jaji Mkuu ni nyeti, hivyo uteuzi wake unahitaji umakini ili kuteua Jaji ambaye ataleta mapinduzi ya kweli katika eneo la haki kwa Watanzania. “Nilipoingia madarakani ilikuwa ni kipindi kidogo tu Jaji Mkuu aliyekuwepo Othman Chande alistaafu, sikuwa na historia ya majaji wengi, nikaona nijipe muda kwanza na kuamua kutumia kifungu cha Katiba kilichopo kinachoniruhusukuteua Kaimu Jaji Mkuu,” alieleza.
Alisema katika kipindi hicho hakutaka kuteua jaji ambaye baada ya miaka miwili au mitatu, analazimika kuteua jaji mwingine au jaji aliyepo baada ya muda mfupi anastaafu. “Nilitaka kuteua jaji mwenye sifa ninazozitaka ambaye anaweza kushika nafasi hiyo hata kwa miaka kumi,” alieleza. Pamoja na hayo, Rais Magufuli alisema alitumia muda mwingi kuchekecha aina na sifa ya Jaji Mkuu anayemtaka ikiwemo namna anavyolichukulia suala zima la rushwa kutokana na ukweli kuwa tatizo la rushwa nchini bado ni kubwa na kila mahali lipo.
Alisema hata baada ya kuchaguliwa na Watanzania kuwa rais wao, alikuwa akimuomba Mungu kila siku ampatie kiongozi atakayemsaidia kulisimamia tatizo hilo la rushwa ipasavyo. Alisema na katika kuhakikisha anapata mtu mwenye sifa hizo, na katika uchambuzi wake wa majaji waliopo nchini, Profesa Juma alimuidhinisha kuwa na sifa hizo ikiwemo uwezo na weledi wake katika utendaji. “Awali nilipokuteua kuwa Kaimu Jaji Mkuu walikuponda sana, walisahau kama kuna kifungu kwenye Katiba kinachonipa mamlaka ya kufanya hivyo, sasa sijui hawa hawakusoma sheria? Ila nashukuru ulikuwa mvumilivu na ukakaa kimya,” alisema.
Aliwataka Watanzania kutambua kuwa kazi ya Jaji Mkuu ni ngumu kwani inagusa maeneo mengi ya haki, ikiwemo kutoa hukumu ngumu kama vile kunyonga ambazo mwisho wa siku wanasiasa ndiyo huwa wa mwisho kuidhinisha mtu afe au la. “Naona nimeletewa orodha ndefu ya wafungwa wanaotakiwa kunyongwa, nawaomba kabisa msiniletee kwa sababu najua ugumu wake...,” alisema. Alipongeza majaji wote nchini kwa kazi nzuri wanazofanya katika kuwapatia haki Watanzania, lakini pia kuendeleza uadilifu wao hata pale wanapostaafu.
“Mnaona hapa leo wapo majaji wengi tu wastaafu kutokana na uadilifu wao, hatujawahi kusikia wanasema chochote, ila wale wastaafu wa sekta nyingine zile wanawashwawashwa. Hawa hawasemi chochote kwa sababu wanajua sheria,” alisema. Pamoja na hayo, Dk Magufuli alizungumzia changamoto zinazoikabili sekta ya mahakama nchini ikiwemo bajeti ndogo, uteuzi wa majaji ambao kwa sasa wengi wao wamestaafu, marupurupu ya majaji pamoja na usafiri.
Alisema si sekta hiyo pekee kwa sasa inayokabiliwa na changamoto mbalimbali kwani hata Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), magereza, uhamiaji na zimamoto zote zinakabiliwa na changamoto ambazo serikali inazifanyia kazi. Aidha, aliviagiza vyombo vyote vya ulinzi nchini ikiwemo PCCB kukutana kwa pamoja na kujadili changamoto zinazovikabili vyombo hivyo hasa zile zinazoingiliana na kuangalia namna bora ya kuzishughulikia kwa faida ya Watanzania.
Kwa upande wake, Profesa Juma, pamoja na kumshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini na kumpatia wadhifa huo nyeti, pia alianika mikakati yake ya namna ya kuboresha sekta ya Mahakama ikiwemo kupunguza tatizo la uhaba wa majengo ya Mahakama na kukarabati yale yaliyochakaa. Alisema wakati akikabidhiwa ofisi na Jaji Mkuu Mstaafu Chande, alimkabidhi taarifa inayoonesha hali halisi ya Mahakama nchini ikiwemo uhaba mkubwa wa Mahakama za Mwanzo, wilaya na Mahakama Kuu katika maeneo mengi Tanzania Bara.
Alisema hadi sasa Tanzania ina jumla ya kata 4,000, lakini kati ya kata hizo ni kata 976 tu ndiyo zenye mahakama hizo ambapo kwa upande wa Dar es Salaam pekee, kuna jumla ya kata 89 na kati ya hizo ni kata 12 tu ndiyo zenye Mahakama za mwanzo hivyo zinahitajika mahakama 77. Kwa upande wa halmashauri za wilaya ambazo zipo 139, ni halmashauri 113 ndiyo zenye Mahakama za Wilaya na nyingi zenye mahakama hizo majengo yake yako kwenye hali mbaya.
Akizungumzia Mahakama Kuu, Jaji Juma alisema Tanzania Bara kuna mikoa 26, kati ya mikoa hiyo 12 bado haina majengo ya Mahakama Kuu na baadhi ya mikoa majengo yake yaliyopo ni mabovu. Alielezea kuwa ataendeleza jitihada zilizoanzishwa na majaji wenzake waliopita ikiwemo kutekeleza mradi wa uboreshaji wa mahakama baina ya Tanzania na Benki ya Dunia ambao unatarajia kujenga nchi nzima Mahakama Kuu zitakazokuwa na mitambo ya kisasa.
Alisema chini ya mradi huo, yatajengwa majengo ya Mahakama Kuu katika mikoa ya Kigoma, Morogoro, Singida, Mara, Dodoma na Mwanza na baadhi ya majengo hayo yanatarajiwa kukabidhiwa rasmi mwaka huu. Pamoja na hayo, alisema atahakikisha anafanya kazi kwa kushirikiana na wafanyakazi wenzake na lengo lake ni kuhakikisha mahakama zote nchini zinajiendesha kwa kuzingatia haki na uwazi ili kurejesha imani ya Watanzania kwa vyombo hivyo vya haki.
Aidha, alizungumzia suala la mgongano wa kimaslahi baina ya mihimili mitatu kwa maana ya Mahakama, Bunge na Serikali Kuu na kueleza kuwa mpaka sasa tangu ashike wadhifa wa Kaimu Jaji Mkuu miezi tisa iliyopita, hajaona muingiliano wowote wa kimaslahi zaidi ya kila mhimili kutekeleza wajibu wake. Alisema katika kuhakikisha suala hilo, halijitokezi Mahakama imejipanga kupitia vipaumbele vya serikali ya awamu ya tano katika eneo la sheria ambapo hadi sasa imebaini kipaumbele kikubwa ni kupambana na rushwa, migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji na ujenzi wa miundombinu.
“Kupitia vipaumbele hivyo, na sisi tutajipanga kwenda na kasi hiyo kwa kuwa tayari kushughulikia kesi zote zinazohusu maeneo hayo kwa haraka na weledi,” alieleza. Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alimshukuru Rais Magufuli kwa kumteua Jaji Juma kushika wadhifa huo na kumuelezea kuwa ni mtu anayestahili kutokana na uzoefu wake katika masuala ya sheria.
“Nilimfundisha pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anaonekana mpole, lakini si dhaifu, hata kipindi kile nilipokuwa kijana ilibidi nijiandae ndipo niende darasani vinginevyo angeniumbua. Ana uwezo na najua ataweka mbele maslahi ya Watanzania,” alisema.
Pamoja na hayo, alifafanua juu ya uamuzi wa Dk Magufuli kuchelewa kuteua Jaji Mkuu, tangu Jaji Chande astaafu na kubainisha kuwa si Tanzania pekee iliyowahi kukaa muda mrefu bila nafasi hiyo kuzibwa na kutaja nchi kama Nigeria na Zambia ambazo zilikaa zaidi ya mwaka mmoja Idara ya Mahakama ikiwa chini ya Kaimu Jaji Mkuu. Kuteuliwa na kuapishwa kwa Jaji Juma, kunamfanya kuwa Jaji Mkuu wa sita mzalendo na Jaji Mkuu wa nane kuwahi kushika wadhifa huo nchini tangu Uhuru.