FIGHT FOR FREEDOM

FIGHT FOR FREEDOM

Wacomoro waokotwa wakiwa hana fahamu




RAIA wawili wa Comoro, wameokotwa katika bahari ya Zanzibar wakiwa hawana fahamu baada ya kupotea kwa siku 17 wakiwa kwenye shughuli za uvuvi.
Katika kipindi chote Wacomoro hao walikuwa wakiishi kwa kula samaki wabichi na maji chumvi.
Watu hao ni Mohamed Ali Rashid (35) na Mohamed Said Swalim (37) ambao wamelazwa katika hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa matibabu, huku wakiwa na majeraha sehemu mbali mbali za mwilini mwao.
Watu hao waliokotwa na wavuvi na kufikishwa hospitali wakiwa hali mbaya.
Akizungumza na Zanzibar Leo, Muuguzi wa kitengo cha dharura katika hospitali hiyo, Asia Imamu Shafi, kwa kushirikiana na daktari wa kitengo hicho, Rashid Hassan Ali, alisema watu hao walifikishwa katika hospitali hiyo Juni 13 mwaka huu saa 1.45 asubuhi  wakiwa hawana fahamu.
Alisema baada ya kufikishwa hapo walipatiwa huduma ya kwanza jambo lililowafanya kupata fahamu lakini walishindwa kujieleza kutokana na kutojua lugha yoyote zaidi ya kingazija.
“Ilishindikana kuwatambua kwa haraka kutokana na kuwa walikua hawajui kuzungumza Kiswahili wala Kiingereza lakini kwa bahati nzuri alitafutwa mfanyakazi mwenzetu anaefahamu lugha yao ndipo akawa mkalimani wetu na hapo ndipo tulipoanza kutambua kilichowasibu,” alisema.
Alisema katika uchunguzi wa awali walibaini watu hao walikua wakisumbuliwa na njaa kali kutokana na kuishi baharini siku 17, huku wakila samaki wabichi na kunywa maji chumvi baada ya boti yao ya uvuvi kuharibika.
Nae, Dk. Juma Salum Mambi, alisema timu ya madaktari ya hospitali ya Mnazimmoja kwa kushirikiana na kitengo cha ustawi wa jamii, tayari wamewapatia msaada wa vitu mbali mbali zikiwemo nguo na chakula huku wakiendelea kupatiwa matibabu.
Nae, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir, alisema walipokea taarifa ya kuokotwa raia hao wa kigeni Juni 13 katika ufukwe wa bahari ya Malindi wakiwa wamepoteza fahamu.