Saturday 17 June 2017

‘Tusisubiri fedha za wazungu kupinga udhalilishaji’




MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman, ameitaka jamii kuacha kutegemea fedha za wafadhili (wazungu) katika kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji.
Alisema vitendo hivyo vimekuwa vikikwamisha maendeleo ya jamii hususani mtoto wa kike hali ambayo inachangia kudumaza harakati zao za kiuchumi.
Kauli hiyo aliitoa wakati akifungua kongamano la madhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika lililofanyika ukumbi wa Kilimo Weni, Wete.
Alisema watoto wanahitaji kulindwa, kuhemishiwa na kuthaminiwa jambo ambalo litawawezesha kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu, afya na kushirikishwa katika ngazi za maamuzi.
“Watoto wengi wamekuwa wakikosa haki zao za msingi kutokana na kuendelea kudhalilishwa, hivyo ni jukumu la jamii kuhakikisha wanalindwa, kuthaminiwa na kuheshimiwa,”alisema.
Mapema Mkuu wa wilaya ya Wete, Rashid Hadid Rashid, alisema takwimu za vitendo vya udhalilishaji zinaonesha watoto na watu wenye ulemavu wamekuwa wakifanyiwa unyanyasaji ikiwemo ya kulawitiwa.
Alisema madhila yanayowapata yanaweza kudhibitiwa na kukomeshwa iwapo kila mmoja atawajibika kwa mujibu wa nafasi yake.
Akitoa maelezo mafupi juu ya kongamano hilo, Ofisa kutoka Shirika la Action Aid Pemba, Omar Ali Salim, alisema, shirika hilo limekuwa likishirikiana na wadau wengine wanaoendesha mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.
Kongamano hilo limeandaliwa kwa pamoja kati ya Jumuiya wa Wanawake Mkoa wa Kaskazini Pemba na Shirika la Action Aid likiwa na kauli mbiu ya ‘Tumwendeleze, tumlinde, tumwezeshe na tumpe fursa sawa mtoto’.

No comments:

Post a Comment

nice